Habari

Migogoro ya Mipaka ya Vijiji 10 yatatuliwa Tandahimba

Migogoro ya Mipaka ya Vijiji 10 yatatuliwa Tandahimba
May, 20 2025

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mtwara imefanikiwa kutatua migogoro ya mipaka ya Vijiji zaidi ya 10 wakati wa zoezi la uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji katika Wilaya hiyo.

Akizungumzia zoezi hilo, Mpima ardhi kutoka Tume Bw. Mikidadi Kalimang’asi ameeleza kuwa, uwepo wa migogoro hiyo umechangiwa na vyanzo mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi juu ya maeneo halisi ya Vijiji vyao vinapogawanyikia hali inayosababisha kuwepo kwa mivutano ya mara kwa mara juu ya mipaka hiyo.

Bw. Kalimang’asi amesema kuwa, wakati mwingine kuibuka kwa migogoro hiyo kunachangiwa na kugombania maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji mali kama vile Kilimo au Biashara ambapo Kijiji kimojawapo kinachokosa maeneo kama hayo hulazimisha kuyapata kwa kuzua mgogoro wa mpaka.

Aidha Mpima Ardhi huyo ameeleza njia mbalimbali wanazotumia kutatua migogoro hiyo kwa mujibu wa Sheria ikiwemo ushirikishwaji wa wananchi wa Vijiji husika kwa kuwa wao ndio wanaufahamu mpana wa maeneo wanayoishi na kufanya shughuli zao za kila siku.

Migogoro ya Mipaka ya Vijiji iliyotatuliwa na kupekelea kuhuishwa kwa mipaka ya Vijiji hivyo ni Bandari dhidi ya Shangani, Mihambwe na Ruvuma, Mkaha na Kisagani pamoja na Chikongo dhidi ya Misufini.

Vijiji vingine vilivyotatuliwa migogoro na kuhuishwa mipaka yao ni Dinyeke dhidi ya Naputa Sokoni, Maundo na Kunandundu, Chiumo na Naputa Shuleni, Chiumo na Naputa Sokoni pamoja na Namahonga dhidi ya Pachani.

Aidha, katika hatua nyingine, jumla ya Vijiji vinne (4) vimepimwa upya mipaka inayovitenganisha (sub division) mara baada ya Vijiji hivyo kugawanyika na kuzaa Vijiji vingine. Vijiji vilivyopimwa upya mipaka inayowatenganisha ni Namahonga dhidi ya Chang’ombe pamoja na Michenjele dhidi ya Bandari.

Wataalamu kutoka Tume wapo katika hatua za mwisho kuwezesha zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 16 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba kupitia Programu ya Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Vijiji ambayo inaendelea katika Halmashauri nyingine 20 nchini.