Habari

Mkurugenzi Mkuu akagua Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Gairo

Mkurugenzi Mkuu akagua Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Gairo
Oct, 22 2025

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bw. Joseph C. Mafuru, leo tarehe 22 Oktoba 2025, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Mkoani Morogoro, kwa ajili ya kukagua kazi ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 16 inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya hiyo.

Akiwa katika ziara hiyo, Bw. Mafuru alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Bi. Sharifa Nabalang’anya, ambapo walikubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya Tume na Halmashauri hiyo ili kuhakikisha Vijiji vingine navyo vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya maendeleo ya Wananchi, Wilaya na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Bi. Nabalang’anya aliishukuru Tume kwa kuwezesha utekelezaji wa zoezi hilo, akibainisha kuwa kwa kipindi cha muda mrefu kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ilikuwa na Vijiji vinne tu vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mkurugenzi huyo amesema kwa sasa kutokana na ujio wa zoezi hilo, idadi ya Vijiji vitakavyokuwa vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi vitaongezeka maradufu, hatua itakayosaidia kuweka msingi thabiti wa matumizi bora ya rasilimali ardhi na kupunguza migogoro baina ya makundi mbalimbali.

Wakati akiendelea na ziara yake uwandani katika Vijiji vya Ihenje na Idibo, Bw. Mafuru alikutana na wataalamu wa Tume, Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji, pamoja na Kamati za Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi za Vijiji hivyo na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa kazi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuwapongeza wataalamu kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuendelea kuwa na weledi, uadilifu, na uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo inayosimamia sekta ya upangaji matumizi ya ardhi.

Aidha, Bw. Mafuru alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi katika kazi hizo, akibainisha kuwa mipango ya matumizi ya ardhi ni nyenzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu Vijijini ambapo wananchi ndio mdau namba moja katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Kazi kama hiyo pia inaendelea katika Halmashauri nyingine nne za Nzega, Mtwara, Mbogwe na Kilolo, ambapo jumla ya Vijiji 74 vinaandaliwa mipango yao kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini, unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia fedha za miradi ya maendeleo.