Habari

Tume yashiriki Mkutano wa COP30 – Brazil

Tume yashiriki Mkutano wa COP30 – Brazil
Nov, 13 2025

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) ni miongoni mwa Ujumbe kutoka Tanzania unaoshiriki katika Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) mjini Belém, Brazil kuanzia Novemba 10 – 21, 2025.

Katika Mkutano huo, Tume inalenga kuwasilisha hatua zilizopigwa na Tanzania katika kuimarisha upangaji wa matumizi ya ardhi, usimamizi wa rasilimali asilia na uhimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Tume pia itashiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu nafasi ya sekta ya ardhi katika kupunguza hewa ya ukaa na kuboresha usalama wa mazingira.

Kupitia ushiriki wake, Tume intarajia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika nyanja za upangaji wa ardhi, matumizi ya teknolojia za kidijitali, pamoja na upatikanaji wa fedha za kimataifa za mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya matumizi endelevu ya ardhi nchini.

Aidha, Tume itatumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na Taasisi za kimataifa na nchi wanachama kuhusu mbinu bora za kusimamia rasilimali ardhi na uhifadhi wa mazingira yanayoharibika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Matokeo yanayotarajiwa kutokana na ushiriki wa Tume katika COP30 ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano wa kimataifa, upatikanaji wa rasilimali kifedha zitakazosaidia kuboresha mifumo ya upangaji wa matumizi ya ardhi nchini na kuhakikisha ardhi inatumika kwa njia endelevu, jumuishi na yenye tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.