Habari
Programu ya KKK kupunguza Migogoro ya Ardhi

WANMM
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia Programu ya Kupanga, Kupima na kumilikisha ardhi nchini ili kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kuipa thamani ardhi kuwa mtaji kwa wananchi kuweza kukopesheka na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Mhe. Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ofisi yake Aprili 09, 2025 Bungeni jijini Dodoma kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026.
Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025, Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha imepima viwanja 7,550 katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma na Njombe. Kwenye eneo la upangaji wa miji, michoro ya mipangomiji yenye viwanja 126,935 imeidhinishwa na hati miliki za viwanja 3,569,994 kubadilishwa kuwa za kidijiti.
Aidha, amesema Serikali imeendelea na utekelezaji wa Programu ya Kurasimisha Makazi na Kuzuia Makazi yasiyopangwa maeneo ya mijini na imeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 4,346 na kupima mipaka ya vijiji 10,744 kati ya 12,318.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuboresha Mfumo wa Kielektroniki wa e-Ardhi wa utunzaji taarifa za ardhi, ambapo mfumo huo unatumika katika mikoa 7 ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Shinyanga, Tabora, Pwani na Mtwara na Halmashauri 20. Kupitia mfumo huo, jumla ya hatimiliki 863 zimesajiliwa.
Kadhalika Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi 5,000 za gharama ya kati na chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme ambapo Dar es Salaam zitajengwa nyumba 2,500 na tayari ujenzi wa nyumba 560 unaendelea na umefikia asilimia 80, Dodoma nyumba 1,000 na mikoa mingine nyumba 1,500.
Katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi; Kuandaa na kukamilisha Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kwa Vijiji vilivyosalia; na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kuongeza ufanisi wa kazi ikiwa pamoja na uhifidhi wa nyaraka mbalimbali za ardhi.