Habari
Tanzania yatoa wito wa Kimataifa kusaidia Upangaji Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi kwa Uhimilivu wa Tabianchi – COP30
Belem, Brazil
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza wigo wa Upangaji Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi (Participatory Land Use Planning) kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda ikolojia muhimu na kuhakikisha usalama wa umiliki wa ardhi.
Akizungumza katika mjadala wa pembezoni uliofanyika wakati wa Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Constantine Mafuru, alisema kuwa Upangaji Shirikishi wa Matumizi ya Ardhi umethibitishwa kuwa mojawapo ya mbinu madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na usimamizi endelevu wa rasilimali za ardhi.
Bw. Mafuru ameeleza kuwa Tume imekuwa mstari wa mbele katika kuratibu Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa katika malengo ya Kitaifa ya Usawa wa Uharibifu wa Ardhi (LDN) na Michango ya Kitaifa Iliyopangwa ya Kupunguza Athari za Tabianchi (NDCs).
Aidha, katika wasilisha lake, Mkurugenzi Mafuru amesisitiza kuwa upangaji wa matumizi ya ardhi sio tu chombo cha kupanga ardhi, bali ni nguzo ya uhimilivu wa tabianchi, usalama wa umiliki, na maendeleo jumuishi Mijini na Vijijini kwani Mipango hiyo husaidia wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo kinachohimili tabianchi, upandaji miti, hifadhi ya misitu, malisho, makazi na maeneo oevu.
Akitoa takwimu za upangaji matumizi ya ardhi kwa Ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF), alisema kuwa, Tume imewezesha kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 60, Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) 6,550 zilizochangia kuimarisha usalama wa ardhi na uwekezaji kwa wananchi hali iliyopelekea kuongezeka kwa idadi ya Vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi kufikia 4,832 sawa na 39.18% mwaka 2025.
Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa fedha, uwezo wa kiufundi, mahitaji ya teknolojia za kisasa kama GIS na mifumo ya kuhifadhi na kuchakata taarifa pamoja na fedha nyingi za miradi kuelekezwa kwenye Wilaya chache za majaribio badala ya kufikia nchi nzima kunapunguza kasi ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi Mafuru alifafanua kuwa, hadi sasa Vijiji 7,501 bado havijandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ambapo ilielezwa kuwa ni takwa la dharura linalohitaji uwekezaji wa pamoja kutoka kwa Serikalini, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ili kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchi nzima hali itakayosaidia uhifadhi wa mazingira kuwa endelevu.
Ili kukabiliana na changamoto hizo Bw. Mafuru alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau kuchangia juhudi za Tanzania kwa kujenga ushirikiano mpana Kimataifa, kuanzisha Mfuko maalum wa kugharamia upangaji wa matumizi ya ardhi na kutekeleza Mpango Mkakati unaohitaji takribani Dola za Marekani milioni 145 (Bilioni 357) ili kukamilisha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji nchi nzima.
Bw. Mafuru alihitimisha kwa kusema kuwa uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi unaanzia kwenye ardhi, endapo itapangwa vizuri sasa, tutajenga mustakabali endelevu kwa vizazi vijavyo na kutakuwa jamii yenye uwezo wa kustahimili na kukabiliana na tabianchi, usalama wa chakula, na uhifadhi wa mazingira.
Mjadala huo ulivutia wataalamu wa mazingira, Serikali, washirika wa maendeleo na Taasisi za utafiti kutoka Mataifa mbalimbali, ambao walijadili na kusisitiza umuhimu na faida za upangaji wa matumizi ya ardhi kama suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
