Habari

TEHAMA yatajwa Kurahisisha Upatikanaji wa Hati

TEHAMA yatajwa Kurahisisha Upatikanaji wa Hati
Mar, 12 2025

Mfumo wa kielektroniki wa Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUIS) uliotengenezwa na Tume umetajwa kuwa nyenzo muhimu inayorahisiha utambuzi wa maeneo ya wananchi, kuyapima na kuyamilikisha Kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs).

Hayo yamebainishwa na Suzana Mapunda, Meneja wa Kanda ya Kati kutoka Tume wakati wa halfa ya ugawaji Hati kwa wananchi 360 wa Kijiji cha Mpinga kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma.

“Hatimiliki hizi tumeziandaa kwa muda mfupi sana, tumeweza kufanya hivyo kutokana na Tume kuwa na Mfumo wa utunzaji data, Mfumo huu umetuwezesha kukusanya taarifa za wamiliki wa vipande vya ardhi, kuchakata kwa haraka na kutoa rasimu ya Hati hapo hapo”, alisisitiza Bi. Mapunda.

Awali, akitoa taarifa ya zoezi la uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi Wilayani hapo, Bi. Mapunda alieleza kuwa, katika awamu hii, jumla ya Vijiji 10 vimewezeshwa kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ambapo wananchi wa Vijiji hivyo wameweza kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo malisho, kilimo, uwekezaji, makazi na mengineyo kulingana na mahitaji yao na uwezo wa ardhi katika Vijiji husika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Zaina M. Mlawa, amewataka wananchi walionufaika na Hati hizo kuzitunza na kuzitumia vizuri, pia wasisite kuomba ushauri kwa wataalamu wake pindi watakapotaka kujikwamua kiuchumi kupitia Hatimiliki hizo.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walionufaika na Hati hizo, wameishukuru Serikali kwa kuwamilikisha maeneo yao, na kusema kuwa kuanzia sasa, kila mtu atajua mwanzo na mwisho wa umiliki wa eneo lake hali itakayosaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima iliyokuwa ikiibuka mara kwa mara.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bahi akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Joachim Thobias Nyingo ambaye ndiye alikuwa Mgeni rasmi. Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya Comrade Masima, Mhe. Mbunge wa Jimbo la Bahi Mhe. Kenneth Nollo na Diwani wa Kata ya Mpinga Mhe. Kudagana Ndalu.