Habari
Tume, Wami/Ruvu kushirikiana katika Upangaji na Usimamizi Matumizi ya Ardhi

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Kanda ya Mashariki leo Machi 26, 2025 imekutana na kufanya mazungumzo na Manejimenti ya Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu (WRBWB) yenye lengo la kuimarisha mashirikiano ya utekelezaji kazi baina ya Taasisi hizo mbili kwenye nyanja ya Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Matumizi ya Ardhi katika maeneo yanayosimamiwa na Bonde hilo.
Pamoja na masuala mengine, mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Ofisi za Bonde la Wami/Ruvu Mkoani Morogoro, yalijikita katika kuangalia Maeneo ya Ushirikiano, na Kupanga Mikakati ya Pamoja Katika Kuimairisha Ushirikiano baina ya Taasisi hizo kwa manufaa mapana ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa Tume uliongozwa na Mkuu wa Kanda ya Mashariki Bw. Edward Mpanda aliyeambatana na Wataalamu mbalimbali waliopo Mkoani Morogoro, Makao Makuu ya Ofisi za Tume Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Pwani, Dar es Salama na Morogoro.
Ofisi ya Wami/Ruvu wameishukuru Tume kwa hatua hiyo na kuahidi kuimarisha ushirikiano katika utendaji kazi huku Ofisi hiyo ikiomba takwimu za Vijiji kwenye ukanda huo na kuona namna watakavyoshirikiana na Tume katika kuwezesha usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji katika maeneo ya hifadhi wanayoyasimamia