Habari
Tume yabisha hodi Kibiti

Na Moteswa Msita
Baada ya kukaa muda mrefu bila kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji, hatimaye Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti iliyopo Mkoani Pwani, imepata neema ya Vijiji vyake 9 kuwezeshwa kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project).
Wakizungumza mara baada ya kuwapokea wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), wanaowezesha zoezi hilo, baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Pwani wakiwemo Katibu Tawala Mkoa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Mkoa wameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa Halmashauri ya Kibiti kunufaika na uandaaji wa mipango hiyo.
Viongozi hao kwa nyakati tofauti, wameitaka Tume kuendelea kufanya mawasiliano ya karibu na ofisi za Mikoa ili kufanikisha utekelezaji wa zoezi hilo. Vilevile, Viongozi hao wamesisitiza juu ya kuwajengea uwezo wataalamu wa Halmashauri ili waweze kuendelea na zoezi kama hilo pindi wataalamu wa Tume wanapoondoka.
Aidha kwa upande wao Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Denis Kitali wamefurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na Serikali kuwezesha zoezi la uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi kwa vijiji hivyo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa Tume ili kufanikisha zoezi hilo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Wilaya.
Kiongozi wa timu ya wataalamu iliyopo Kibiti, ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Mashariki Bw. Edward Mpanda ameeleza kuwa zoezi hilo ni Shirikishi kwa maana ya kila ngazi kuanzia Mkoani hadi Vijijini wanapaswa kufahamu utekelezaji wa zoezi hilo huku akiwaasa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu ili kuwezesha utekelezaji wa kazi hiyo.
Vijiji vitakavyonufaika na zoezi hilo katika Wilaya ya Kibiti ni Mkupuka, Machipi, Mlanzi, Ngondae na Nyanjati. Vijiji vingine ni pamoja na Hanga, Nyakinyo, Tomoni na Mangwi.