Habari
Umuhimu wa Kuhakiki na Kuhuisha Mipaka kati ya Vijiji wakati wa Uandaaji Mipango ya Matumizi Ya Ardhi
Wakati wa uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika ngazi ya Vijiji, suala la kuhakiki mipaka kati ya Kijiji na Kijiji kingine ni hatua muhimu inayochangia katika kuhakikisha mipango hiyo inakuwa sahihi, halisi na inatekelezeka.
Endapo, mipaka hiyo itakuwa haiendani na uhalisia au uwepo wa Vijiji vilivyogawanyika, mipaka hiyo inabidi ihuishwe ili kuondoa migongano. Kuhuisha mipaka kunalenga kuhakikisha kuwa mipaka yote inatambuliwa kisheria, inaheshimiwa na pande zote, na inakuwa rejea sahihi wakati wa upangaji, usimamizi na utekelezaji mipango ya matumizi ya ardhi.
Aidha, uhakiki na uthibitisho wa mipaka husaidia kuondoa migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza kati ya Vijiji jirani, hasa pale ambapo mipaka haijawahi kuainishwa au imesahaulika kutokana na mabadiliko shughuli za kiuchumi au mgawanyo wa Vijiji. Kwa kufanya hivyo, jamii hupata uelewa wa pamoja kuhusu eneo lao halisi na matumizi yaliyokusudiwa, jambo ambalo linajenga misingi ya amani, ushirikiano na maendeleo endelevu.
Kuhuisha mipaka pia huongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii, uwekezaji, kilimo, na hata uhifadhi wa mazingira. Halmashauri za Vijiji hupata urahisi wa kupanga matumizi ya ardhi kwa uwiano unaozingatia rasilimali zilizopo na mahitaji ya kijamii na kiuchumi.
Hii husaidia pia katika utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs), kwani mipaka iliyothibitishwa hutoa uhakika wa umiliki kwa wananchi pindi inavyokuja hatua ya kuhakiki maslahi ya ardhi kwa mwananchi mmoja mmoja na kuhakikisha wanamilikishwa ndani ya mipaka ya Kijiji husika.
Kwa ujumla, kuhakiki na kuhuisha mipaka kati ya Vijiji ni hatua ya msingi katika kuhakikisha kuwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi inakuwa nyenzo madhubuti ya kusimamia, kulinda na kuendeleza rasilimali ardhi kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Ni muhimu zoezi hili lifanyike kwa ushirikishwaji wa jamii, uwazi, na kwa kuzingatia Sheria na Miongozo ya Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini.
