Habari

Vijiji 16 Gairo vyanufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi

Vijiji 16 Gairo vyanufaika na Mipango ya Matumizi ya Ardhi
Oct, 22 2025

Vijiji 16 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Mkoani Morogoro, vimenufaika na utekelezaji wa mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) unalenga kuboresha matumizi ya rasilimali ardhi Vijijini na kuepusha migongano ya shughuli za uzalishaji kama kilimo, ufugaji, makazi na uhifadhi wa mazingira.

Wakazi wa Kijiji cha Lukando wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo, wakisema kuwa kukamilika kwake kutasaidia kumaliza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Bi. Magreth Elibariki Msuya, amesema kuwa kupitia mpango huo, idadi ya Vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi itaongezeka kutoka vinne vya awali hadi kufikia Vijiji 20. Amesema hatua hiyo itasaidia Wilaya kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi inayozingatia maendeleo endelevu.

Aidha, Joseph Mbilinyi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi makao Makuu Dodoma, amesema kuwa upangaji wa maeneo utasaidia Vijiji kuwa na matumizi sahihi ya ardhi, kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuweka suluhu ya kudumu kwa migogoro ya ardhi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Bi. Sharifa Nabalang’anya, amesema kuwa maeneo yatakayopimwa kwa awamu hii yako katika mpango thabiti wa kilimo cha mazao mapya, hatua itakayoongeza kipato na kukuza uchumi wa wananchi wa Gairo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Katibu Tawala wa Wilaya amesisitiza kuwa zoezi hilo halitakuwa na tija endapo mipango haitasimamiwa ipasavyo. Amesisitiza viongozi wa Vijiji na vitongoji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo na kutoa ushirikiano kwa timu ya wataalamu wanaowezesha zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi.