Habari

Wananchi 1500 kunufaika na Hatimiliki za Kimila kwenye Mikoa 6

Wananchi 1500 kunufaika na Hatimiliki za Kimila kwenye Mikoa 6
Feb, 14 2025

Zaidi ya Wananchi 1500 waliopo katika Halmashauri za Wilaya sita za Mikoa ya Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma na Geita wanatarajiwa kuwezeshwa kumiliki ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) mara baada ya Vijiji hivyo kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi zoezi lililoanza Februari 12, 2025 kwenye Vijiji hivyo.

Akizungumza katika Kikao Kazi baina yake na Wataalamu wa Tume wanaokwenda kuwezesha zoezi hilo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya husika, Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph Mafuru amewataka Wataalamu hao kufanya kazi kwa weledi ili kazi hiyo ilete manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Vilevile, Bw. Mafuru aliongeza kuwa, uandaaji wa mipango hiyo uhusisha sekta mtambuka zinazotumia ardhi, na matokeo yake hutumiwa na wadau mbalimbali katika kutekeleza kazi zao, hivyo ni vyema kuwa makini na kutoa kazi zenye ubora wa kiwango cha juu.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu na kazi hiyo, Mkurugenzi anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu, Bw. Jonas Masingija Nestory amesema kuwa, katika awamu hii, Tume itawezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 57 katika Halmashauri za Wilaya 6 ambapo kati hizo, Vijiji vilivyopo kwenye Halmashauri 5 vitaandaliwa Mipango Kina (Detail land use Plans) na wananchi wake kupatiwa Hatimiliki.

Aidha, Bw. Masingija alifafanua kuwa kufanyika kwa kazi hiyo ni muendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mradi huo umejikita katika kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji vilivyopo kwenye Wilaya zinazopitiwa na Miradi ya Kimkakati kama vile SGR, JNHPP, EACOP, Wilaya zilizopo mipakani na nchi jirani, pamoja na Vijiji vyenye Migogoro ya matumizi ya Ardhi.

Halmashauri za Wilaya zitakazonufaika na zoezi hilo katika awamu hii ni Bahi (Dodoma), Kilolo (Iringa), Mbarali (Mbeya), Mbogwe (Geita), Rombo (Kilimanjaro) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti iliyopo Mkoa wa Pwani.