Habari

Wananchi 600 Sikonge Kunufaika na Hati za Hakimiliki za Kimila

Wananchi 600 Sikonge Kunufaika na Hati za Hakimiliki za Kimila
Apr, 09 2026

Zaidi ya wananchi 600 waliopo katika Vijiji vitatu vya Majojoro, Kapumpa na Muitikio katika kata ya Nufaika, Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kufuatia kuanza kwa zoezi la kuhakiki maslahi ya ardhi na upimaji wa mashamba yao.

Zoezi hilo linalowezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Shirika la Uhifadhi la Association for Development of Protected Areas (ADAP) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, likilenga kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi yao kisheria ili kujikwamua kiuchumi.

Kupitia umilikishaji huo, wananchi watapata fursa ya kutumia Hati hizo kama mtaji wa kuendeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa uyoga kupitia maliasili zilizopo katika Vijiji vyao, hivyo kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Aidha, hatua hiyo inatarajiwa kuondoa migogoro ya ardhi kati ya mtu na mtu, pamoja na kuweka mipaka ya bayana kati ya maeneo ya shughuli za binadamu na yale ya uhifadhi wa misitu, hali itakayochangia kulinda ikolojia na rasilimali za asili.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkuu wa Kanda ya Magharibi kutoka Tume, Bw. Emmanuel Magembe, amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanakuwa na milki salama za ardhi zao, jambo linalochangia kupunguza migogoro na kufungua fursa za maendeleo ya kiuchumi endapo Hatimiliki hizo zitatumika ipasavyo.

“Upatikanaji wa hati hizi za Hakimiliki za Kimila utawawezesha wananchi kutumia ardhi yao kama rasilimali muhimu ya maendeleo, ikiwemo kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji,” amesema Bw. Magembe.

Kwa upande wao, wadau wa maendeleo kutoka ADAP wamepongeza ushirikiano uliopo kati ya Tume na jamii, wakieleza kuwa mpango huo una mchango mkubwa katika kuimarisha usimamizi bora wa ardhi na kuboresha maisha ya wananchi wa Vijijini.

Wamesisitiza kuwa mipango ya matumizi ya ardhi pamoja na utoaji wa Hati Miliki za Kimila ni msingi muhimu katika kuhakikisha matumizi endelevu ya ardhi, amani ya jamii na maendeleo jumuishi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.