Habari
Bahi Wapokea kwa mikono miwili Fursa ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

Halmashauri ya Wilaya ya Bahi iliyopo katika Mkoa wa Dodoma, imeipongeza Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kuwezesha awamu nyingine ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 10 ndani ya Wilaya hiyo.
Hayo yamebainika wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Zaina Mlawa akiongea na Wataalamu kutoka Tume waliopiga kambi Wilayani humo kwa ajili ya kuwezesha zoezi hilo litakaloambatana na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi zaidi ya 300 katika Wilaya hiyo.
“Katika Wilaya yetu ya Bahi, Vijiji 10 vilivyopo kwenye Kata 8 vinaenda kuwezeshwa kuandaa hii mipango, kimsingi hiki kilikuwa ni kilio chetu cha muda mrefu sana, kwa maana sisi kama Halmashauri tumekuwa tukitenga bajeti kwa ajili ya upangaji lakini imekuwa ni kidogo sana, tunashukuru Wizara yetu kupitia Tume imetusikia na kuteletea fedha na wataalamu kwa ajili ya kupanga” alisema Mkurugenzi Mlawa
Aidha, Mkurugenzi Mlawa aliongeza kuwa, Halmashauri yake itatoa ushirikiano mkubwa kuhakikisha lengo linafikiwa kwani upangaji na umilikishaji wa ardhi ni jambo muhimu kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuwa husaidia katika uhifadhi, kuondoa migogoro pamoja kuwa na miji iliyopangwa vizuri hapo baadae pindi Vijiji vinapokuwa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kanda ya Kati kutoka Tume, Suzana Mapunda, ameeleza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi inapitiwa na Mradi wa Kimkakati wa SGR pamoja na Mito inayotiririsha maji kuelekea Mto Ruaha hadi JNHPP hivyo uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi unalenga kulinda na kuhifadhi miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
“Tunapoandaa mipango ya matumizi ya ardhi, tunawahamasisha na kuwawezesha wananchi kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali, kule kwenye maeneo jirani na Miradi ya Kimkakati, tunawashauri na kuwaongoza Kitaalamu kutenga matumizi ya ardhi ambayo ni rafiki na miradi hiyo ili kuleta uendelevu wa ardhi na kutunza mazingira” alisisitiza Bi. Mapunda.
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ina jumla ya Vijiji 59, ambapo hadi zoezi hilo likikamilika, Halmashauri hiyo itakuwa na jumla ya Vijiji 29 vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Kati ya Vijiji hivyo 29, Vijiji 20 vimeandaliwa mipango hiyo kwa kuwezeshwa na Tume kwa awamu tofauti, na vingine 9 ni jitihada za Halmashauri pamoja na wadau wengine.