Habari
Buhigwe mbioni Kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji vyote

Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe iliyopo Mkoani Kigoma, ipo mbioni kukamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji vyote vilivyopo kwenye Wilaya hiyo ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba 2024, jumla ya Vijiji 35 kati ya Vijiji 44 vitakuwa vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
Kukamilika kwa uandaaji wa mipango ya matumizi katika Wilaya hiyo iliyopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Burundi, itasaidia kuwahakikishia wananchi milki salama za ardhi zao pindi watakapopimiwa maeneo yao na kupatiwa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs).
Akizungumza na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) waliofika kwa mara nyingine tena Wilayani hapo kuwezesha uandaaji wa mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji, Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Michael Ngayalina ametambua na kupongeza juhudi za Serikali katika upangaji matumizi ya ardhi maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Vijiji ndani ya Wilaya yake.
“Natambua Serikali inafanya kazi kubwa ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo huwezesha kutatua migogoro ya ardhi, kuweka utaratibu wa namna ya kila sekta kujua inatumiaje ardhi, kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji pamoja na kuweka sawa mipaka ya Vijiji pale ambapo mipaka hiyo haiendani na uhalisia” alisema Kanali Ngayalina.
Aidha, Kanali Ngayalina aliwataka wataalamu hao kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuwafanya waepukane na kusababisha migogoro midogo midogo ambayo hutokea kwa sababu ya kukosa elimu ya ardhi.
Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri hiyo Bw. Ismail Gwasa amesema kuwa baada ya kuona mafanikio ya mipango ya matumizi ya ardhi iliyoandaliwa awali, na kwa kuwa Halmashauri hiyo ipo mbioni kuanza kupima na kumilikisha ardhi, iliwalazimu kuwaandikia Tume kuomba kuwezeshwa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji vilivyosalia.
“Halmashauri ina lengo la kuanza kupima viwanja na mashamba na kuwamilikisha wananchi, ili tuweze kufanya hivyo kwenye Wilaya yote, hatuna budi kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwanza, kwani ndio nyenzo muhimu na dira itakayotupelekea kufanya upimaji na kumilikisha maeneo kadri yalivyotengwa kwenye mipango” alisisitiza Bw. Gwasa
Katika safari hiyo ya Halmashauri ya Buhigwe kukamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji, jumla ya Vijiji 30 vilivyoandaliwa mipango hiyo vitakuwa vimewezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi wakati vingine 5 vikiwezeshwa na Taasisi ya MKURABITA.
Wakati huo huo, Wataalamu kutoka Tume kwa kushirikiana na Wataalamu wa Halmashauri hiyo, wameanza zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya matumizi ya ardhi katika Vijiji 7 vya awamu ya kwanza kati ya Vijiji 14 vinavyotarajiwa kuandaliwa mipango hiyo.
Akizungumza katika Kijiji cha Kibande wakati akitoa elimu kwa uongozi wa Kijiji pamoja na Wananchi Kijijini hapo kupitia Mkutano wa Kijiji, Afisa Mazingira kutoka Tume Bw. Daniel Ngatunga ameeleza kuwa uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi wa Kijiji utawasaidia wananchi kutumia ardhi yao vizuri bila kuwa na matumizi kinzani.
Aidha, Afisa huyo kutoka Tume alisisitiza kuwa wananchi watapata fursa ya kuangalia hali halisi ya matumizi ya ardhi yaliyopo Kijijini kwao, kufanya tathmini ya matumizi hayo na baadae kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile kilimo, malisho, makazi, maeneo ya huduma za jamii, uwekezaji na nyinginezo kadri ya mahitaji yao.
Kwa upande wao, wananchi wa Vijiji vilivyoanza zoezi hilo wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi huo huku wakiamini kuwa mpango wa matumizi ya ardhi unaenda kuwa suluhisho la migogoro ya ardhi isiyo ya lazima iliyokuwa ikibuka mara kwa mara katika Vijiji vyao.
“Kwanza tunashukuru, maana hapa Kijijini kwetu ardhi iliyopo ni ndogo sana, na watu wanafanya shughuli zao kiholela tu, wengine wanavamia hadi maeneo yaliyokuwa ya Halmashauri ya Kijiji na kuanza kufanya shughuli zao binafsi bila vibali, sasa mwarobaini umekuja, kila kundi la watumiaji ardhi litakuwa linafanya shughuli zao kwenye maeneo yaliyotengwa rasmi” alisema Bw. Atanasi Gwarama, mkazi wa Kijiji cha Kibande.
Zoezi la uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project Na. 4951) linafanyika katika Halmashuri nyingine 6 za Rombo, Nyasa, Busokelo, Nzega, Morogoro pamoja na Mbogwe ambapo linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba.