Habari
Tume yapeleka Tabasamu Halmashauri za Wilaya Saba
Jumla ya Halmashauri za Wilaya saba nchini zimenufaika na uwezeshaji wa uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 40 pamoja na zoezi la Uhakiki wa Maslahi ya Ardhi kwa wananchi takribani 2,400, hatua iliyopelekea wananchi hao kumilikishwa ardhi kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) huku idadi kubwa zaidi ya wananchi imeendelea kujitokeza kushiriki zoezi hilo lilipokuwa likielekea ukingoni.
Hayo yameelezwa Wilayani Ukerewe na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bw. Joseph C. Mafuru, wakati akihitimisha ziara yake ya kukagua utekelezaji wa kazi ya uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji pamoja na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila katika Wilaya za Misungwi na Ukerewe, mkoani Mwanza.
Bw. Mafuru amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Januari, Tume imepokea fedha za miradi ya maendeleo zilizowezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Halmashauri tano, kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa, sambamba na uandaaji wa mipango hiyo, Tume pia imewezesha uandaaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila katika Halmashauri mbili, hatua itakayowawezesha wananchi wa maeneo husika kutumia hati hizo kama dhamana katika taasisi za fedha na kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi hususan kilimo, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja, Vijiji na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia utekelezaji wa zoezi hilo katika Wilaya ya Ukerewe, Bw. Mafuru amesema kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu pamoja na ongezeko la mahitaji ya ardhi, Wilaya hiyo imekuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea migogoro ya ardhi, hali iliyosababisha Tume kuiweka miongoni mwa wanufaika wa mradi huo.
Bw. Mafuru amekiri kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa wananchi wa Ukerewe kuhitaji kumiliki ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa ni kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa kisiwa hicho wananchi wake wanapatiwa fursa ya kumilikishwa ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila.
Hata hivyo, amesema kuwa kutokana na ufinyu wa muda na rasilimali fedha, ni takribani wananchi 1,400 pekee waliofanikiwa kumilikishwa ardhi katika awamu hiyo. Ameahidi kuwa Tume itaendelea kuwahudumia wananchi wengine waliosalia kadri rasilimali zitakavyopatikana, ili kukidhi mahitaji yao na kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wake wa msingi wa kuwahudumia wananchi.
Halmashauri za Wilaya zilizowezeshwa kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji ni Masasi, Kisarawe, Muheza, Mbeya na Misungwi, wakati wananchi wa Halmashauri za Ukerewe na Misungwi waliwezeshwa kuandaliwa Hati za Hakimiliki za Kimila.
Utekelezaji wa kazi hizo umewezeshwa kupitia fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
