Habari

Historia Yaandikwa Ukerewe, Wananchi 1,200 Wamilikishwa Ardhi

Historia Yaandikwa Ukerewe, Wananchi 1,200 Wamilikishwa Ardhi
Jan, 26 2026

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, imeandika historia mpya baada ya kuwawezesha wananchi zaidi ya 1,200 wa Vijiji vya Namagondo na Busiri kumiliki ardhi kisheria kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs). Hii ni mara ya kwanza zoezi la umilikishaji wa ardhi kufanyika katika Vijiji hivyo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia kukamilika kwa uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji na kupitishwa kwa Mipango Kina (Detail Land Use Plans), iliyoweka msingi wa kutambua, kupanga na kurasimisha matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mahitaji ya kijamii, kiuchumi na kimazingira ya wananchi.

Akizungumza wakati wa zoezi la kupitisha Mipango Kina hiyo, Afisa Ardhi Mkuu kutoka Tume, Bw. Otmary Komba, alisema kuwa umilikishaji wa ardhi unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Alifafanua kuwa baada ya Vijiji kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, hufuatiwa na zoezi la utambuzi wa maslahi ya ardhi kwa wananchi, hatua inayowezesha utoaji wa hati za umiliki hususan katika maeneo ya mashamba na makazi.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa zoezi hilo unalenga kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kupunguza migogoro ya ardhi, pamoja na kuwawezesha wananchi kutumia ardhi yao kama rasilimali ya kiuchumi kwa maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Kwa upande wao, wananchi wa Vijiji vya Namagondo na Busiri walieleza kufurahishwa na zoezi hilo, wakibainisha kuwa wamekuwa wa kwanza kumiliki ardhi kisheria miongoni mwa Vijiji vya Wilaya ya Ukerewe, hali inayowapa uhakika wa umiliki na amani katika matumizi ya ardhi yao.

Umiliki wa ardhi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila unatoa fursa kwa wananchi kutumia ardhi kama dhamana katika taasisi za kifedha, kuongeza thamani ya ardhi, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji wa kijamii na kiuchumi Vijijini.

Katika awamu hii, zoezi kama hilo pia limefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jitihada za Serikali kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini kwa kuhakikisha wananchi wanamiliki ardhi kisheria, kulinda rasilimali ardhi, kuondoa migogoro na kuitumia ardhi kama chombo cha kukuza uchumi na ustawi wa jamii.