Habari
Vijiji 8 Kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kulinda Maji na Misitu Mbeya
Katika kuendeleza jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi endelevu wa ardhi na rasilimali za asili, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeanza rasmi zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji nane vilivyopo ndani ya Wilaya hiyo, kwa lengo la kulinda na kutunza vyanzo vya maji, kuimarisha uhifadhi wa misitu, pamoja na kuzuia migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika baadhi ya maeneo.
Zoezi hilo, lililoanza kwa utoaji wa elimu kwa wananchi wa Vijiji husika kuhusu Sheria na miongozo mbalimbali inayosimamia ardhi na rasilimali nyingine, limepokelewa kwa bashasha na wakazi hao, wakieleza matumaini yao kuwa migogoro ya ardhi inayosababishwa na mipaka isiyoeleweka, uvamizi wa maeneo ya hifadhi na matumizi yanayokinzana, itapungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa upande wao, wataalamu kutoka Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wamesema uandaaji wa mipango hiyo utakuwa dira ya matumizi sahihi ya ardhi, huku masuala ya uhifadhi wa mazingira yakipewa kipaumbele cha kipekee. Maeneo yenye vyanzo vya maji, wamesema, yatatambuliwa na kulindwa dhidi ya uharibifu, uchafuzi na uvamizi wa shughuli zisizofaa.
Zoezi kama hilo pia linaendelea kutekelezwa katika Wilaya nyingine nne za Kisarawe, Masasi, Misungwi na Muheza, sambamba na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) zaidi ya 2,400 katika wilaya za Nyang’hwale na Ukerewe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Nchini.
