Habari
Serikali yaendelea Kuchukua Hatua Kudhibiti Migogoro ya Matumizi ya Ardhi Morogoro
Wananchi wa Kijiji cha Muungano, kilichopo Kata ya Lundi, Wilaya ya Morogoro, wamelalamikia kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya ardhi inayotokana na mwingiliano wa matumizi kati ya makundi mbalimbali ya watumiaji ardhi.
Malalamiko hayo yameelezwa mbele ya wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), waliowasili Kijijini hapo kwa lengo la kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji tisa (9) katika eneo hilo.
Wananchi hao wamedai kuwa changamoto kubwa inatokana na kutokuwepo kwa mipaka bayana ya Vijiji jirani pamoja na sintofahamu ya mipaka ya maeneo ya hifadhi, hali inayosababisha muingiliano wa matumizi ya ardhi na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mkuu wa Kanda ya Mashariki kutoka NLUPC, Bw. Edward Mpanda, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti za kudhibiti na hatimaye kumaliza migogoro hiyo kupitia uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Alisema Tume, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, inaendelea na zoezi la kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji ili kuweka mipaka iliyo wazi na kuainisha matumizi sahihi ya ardhi kwa kila kundi la watumiaji.
Baada ya kupatiwa elimu kuhusu umuhimu wa mipango hiyo, wananchi wa Kijiji hicho wameipongeza Serikali kwa kuleta mpango huo kwa wakati muafaka, wakiamini kuwa utasaidia kupunguza migogoro na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo Saidi Nassoro na Frank Amos, walieleza matumaini yao kuwa zoezi hilo litasaidia kuondoa changamoto za muda mrefu za migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
Katika awamu hii, zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi linaendelea pia katika Halmashauri nyingine tatu (3) za Msalala, Rombo na Madaba likihusisha utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) kupitia fedha za miradi ya maendeleo.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuondoa migogoro ya ardhi, kuimarisha uhifadhi wa mazingira, na kuwawezesha wananchi kunufaika kiuchumi kupitia matumizi bora na endelevu ya ardhi.
