Habari
Hati za Hakimiliki za Kimila 1,300 zatolewa Nzega

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imezindua ugawaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila zaidi ya 1,300 kwa Wananchi wa Vijiji vya Seki na Buduba mara baada ya Vijiji hivyo kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji.
Akikabidhi Hati hizo kwa wananchi wachache kwa niaba ya wanufaika wengine 1,353, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nzega ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mh. Mohamed Mussa Mtulyakwaku amewataka wananchi hao kuzingatia masharti ya Hati hizo ili kuepuka migogoro ya umiliki wa ardhi pamoja na kuzitumia kwa malengo mazuri ili ziwasaidie katika kujikwamua kiuchumi.
Mjumbe wa Kamati ya Usimamzi Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji (VLUM) akitoa maelezo ya Ramani ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji cha Buduba iliyoplekea kuandaliwa kwa Hati za Hakimiliki za Kimila katika Kijiji hicho
Aidha, Mh. Mtulyakwaku amegusia umuhimu wa uandaaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji kwani mipango hiyo ni nyenzo muhimu katika Vijiji inayosaidia wananchi kutumia vizuri ardhi yao kwa kuzingatia utaratibu waliojiwekea na kuepukana migogoro isiyo ya lazima.
“Vijiji hivi viwili viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na hatimaye wananchi wake walipimiwa maeneo na kuandaliwa Hati. Hii ni hatua muhimu sana kwani mipango hii ya matumizi ya ardhi huweka utaratibu wa matumizi ya rasilimali za ardhi, kutatua migogoro, kuimarisha miliki salama za ardhi na matumizi yake, sasa nawaasa mkazitumie Hati hizi vizuri ili kuwaletea maendeleo” alisisitiza Mh. Mtulyakwaku.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Nzega ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mh. Mohamed Mtulyakwaku akikabidhi Hati ya Hakimiliki ya Kimila kwa mmoja wa mwananchi wa Kijiji cha Seki
Vilevile, katika hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa Hati hizo uliofanyika leo tarehe 25/10/2025 katika Kijiji cha Seki, Wilayani Nzega, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kuhakikisha kunakuwa na muendelezo wa zoezi hilo kwenye Vijiji vyote vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ili kuwahakikishia wananchi miliki salama za ardhi zao.
“Kwa kuwa Vijiji 31 tayari vimeshaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, naomba nichukue fursa hii kuwaasa Halmashauri ya Wilaya kurudi kwenye Vijiji hivyo na kuendelea na hatua za kuandaa Mipango Kina, kuwapimia wananchi na kuwamilikisha ardhi zao kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila” alisema Mh. Mtulyakwaku
Baadhi ya wananchi wa Vijiji vya Seki na Buduba wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mgeni Rasmi mara baada ya kukabidhiwa Hati za Hakimiliki za Kimila
Akitoa maelezo ya awali juu ya uandaaji wa Hatimiliki hizo, Afisa Ardhi Mkuu kutoka Tume Bw. Otmary Komba amesema kuwa, Hatimiliki hizo ziliandaliwa kufuatia zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 17 lililofanyika Wilayani humo, ambapo Vijiji vya Seki na Buduba viliendelea hadi kwenye hatua ya upimaji na umilikishaji.
“Vijiji vya Seki na Buduba viliandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika hatua zote sita kama zilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Upangaji matumizi ya Ardhi ya Vijiji. Aidha, katika zoezi hilo, jumla ya Hati za Hakimiliki za Kimila 1,353 ziliandaliwa, ambapo Kijiji cha Seki ziliandaliwa Hatimiliki 699 na Kijiji cha Buduba ziliandaliwa Hatimiliki 654” alisema Bw. Komba
Uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji hivyo pamoja Hatimiliki umefanyika kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.