Habari

Idadi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi yaongezeka kwa asilimia 124 – Waziri Ndejembi

Idadi ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi yaongezeka kwa asilimia 124 – Waziri Ndejembi
May, 24 2025

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema idadi ya Vijiji vilivyoandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi imeongezeka kutoka 2,088 mwaka 2021 hadi kufikia 4,679 kufikia Mei 2025.

Amesema ni sawa na ongezeko la vijiji 2,591, ambalo ni sawa na asilimia 124, jambo linalothibitisha jitihada za Serikali katika kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali ardhi nchini.

Ndejembi ameyasema hayo Mei 23, 2025 Jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Serikali imeweka mkazo mkubwa kwenye upangaji wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha matumizi endelevu na yenye tija kwa wananchi. Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Halmashauri, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla,” alisema Mhe. Ndejembi.

Amebainisha kuwa Wizara hiyo imeendelea kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya kimkakati ya kitaifa kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) lenye urefu wa kilomita 1,146 kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga, pamoja na ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR).