Habari

Kamati ya Kitaalamu ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Yaundwa

Kamati ya Kitaalamu ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Yaundwa
Sep, 08 2018

Kamati ya Kitaifa ya Kiufundi inayoundwa na watalaamu kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusiana na matumizi ya ardhi imeundwa. Kamati hiyo imezinduliwa mkoani Morogoro kwa kushiriana na IUCN na OXFAM itakuwa na kazi ya kuishauri Tume juu ya masuala ya kisekta yanayohusu mipango ya matumizi ya ardhi.

Akizindua Kamati hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen Nindi ameitaka Kamati hiyo kuwa chachu ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili matumizi ya ardhi nchini. Aidha, amewataka wajumbe kutumia utaalamu wao kushauri namna sekta hizo zinavyoweza kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha watumiaji wa ardhi wanavyoweza kutumia ardhi vizuri kwa ajili ya uzalishaji.

“Kumekuwapo na changamoto nyingi sana hasa katika suala la migogoro ya ardhi, sasa kwa kuzingatia majukumu yenu kwenye kamati hii, ni wakati muafaka katika kipindi chenu cha miaka mitatu kila sekta itoe ushauri kwa Tume namna gani tunaweza kuondokana na changamoto hizo” alisisitiza Dkt. Nindi.

Kamati hiyo itakuwa na majukumu ya kuanzisha vigezo na taratibu za tathmini ya ubora wa ardhi yote nchini na taratibu za usimamaizi wa rasilimali zinazomilikiwa kwa pamoja. Majukumu mengine ya Kamati hiyo itakuwa ni kushauri juu ya Miongozo na Kanuni za utunzaji wa ardhi endapo ardhi hiyo inahitaji uhifadhi maalumu wa ardhi.

Vilevile, Kamati itakuwa na jukumu la kushauri juu ya miongozo ya maamuzi ya pamoja ya wakala wa upangaji kuhusu masuala yenye umuhimu wa kipekee pamoja na miongozo ya ufuatiliaji na tathmini ya mipango ya matumizi ya ardhi na uidhinishaji wake.

Kamati hiyo imemaliza kikao kazi chake kwa kuweka maazimio yatakayowaongoza kwenye utendaji kazi kwa kipindi watakachokuwepo. Kamati hii inaundwa kwa mujibu wa kifungu namba 19 (5) cha Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Sura 116 ambapo itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.