Habari

Katibu Mkuu Ardhi akagua Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Umilikishaji Ardhi Makete

Katibu Mkuu Ardhi akagua Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi na Umilikishaji Ardhi Makete
Jul, 06 2023

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Antony Sanga ametembelea na kukagua kazi ya uwezeshaji wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 44 katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete na kuhimiza wananchi kujitokeza kwenye zoezi la upimaji mashamba kwa ajili ya kupatiwa Hatimiliki za Kimila.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kigala, Katibu Mkuu amesema kuwa amefika Kijijini hapo kukagua kazi ya kupanga matumizi ya ardhi na kumilikisha ardhi inayowezeshwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

Aidha, Katibu Mkuu ameeleza kuwa kufanyika kwa kazi hiyo ni utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali inavyoelekeza kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ambapo hadi kufikia mwaka 2025 Vijiji visivyopungua 4,000 vinatakiwa viwe vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

“Nimekuja kukagua kazi inayofanyika hapa Kijijini, kwa sasa Serikali inapanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini, Ilani inatuelekeza kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 4,131, na hapa Makete mmebahatika kupata vijiji 44” alisema Mhandisi Sanga.

Vilevile, Katibu Mkuu aliwaasa wananchi wa vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kushiriki kikamilifu na kutoa ushirikiano kwa wataalamu kwenye zoezi la kupimiwa mashamba yao ili kupata Hatimiliki za Kimila ili zitumike kuwaletea maendeleo na kuwainua kiuchumi.

“Kazi kama hii mara nyingi inaishia kwenye kupanga na kupima tu, ila nyinyi mmebahatika zoezi hili linaenda hadi hatua kumilikisha na mtapata Hatimiliki za Kimila ambazo zitawawezesha hata kuchukuliwa mikopo kwenye mabenki ambayo itawasaidia kuwaletea maendeleo” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Hapo awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi hiyo, Mkurugenzi anayeshughulikia Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu kutoka Tume Bw. Jonas Masingija Nestory amesema kuwa, kazi ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ilifanyika kwa kasi na weledi kutokana na ushirikiano wa wananchi vijijini pamoja na viongozi na wataalamu wa Wilaya.

Aidha, alieleza kuwa wakati wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 44, jumla ya mipaka ya vijiji 24 iliweza kuhuishwa ili kuendana na uhalisia wa wananchi wanavyoishi. Pia, katika zoezi hilo jumla ya migogoro ya mipaka ya vijiji 16 iliweza kutatuliwa ikiwemo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi.

“Lakini sambamba na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, kulikuwepo na utatuzi wa migogoro ya mipaka kati ya kijiji na kijiji pamoja na vijiji vilivyokuwa vinapakana na maeneo ya hifadhi ikiwemo Pori la Akiba la Mpanga-Kipengele na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo” alieleza Bw. Masingija.

Vilevile, Mkurugenzi Masingija aliongeza kuwa mara baada ya zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi kukamilika, timu ya wataalamu imeanza kutambua na kupima mashamba ya wananchi kwa ajili ya kuwaandalia Hati za Hakimiliki za Kimila.

Kwa kipindi cha siku 3 toka zoezi la upimaji lianze, wataalamu hao walikuwa wameshapima mashamba zaidi ya 3,000 katika vijiji 5 vya kata ya Ikuwo na Kigala. Aidha, kasi hiyo ya upimaji imetokana na zoezi hilo kufanyika kwa kutumia Mfumo wa Taarifa za Matumizi ya Ardhi (National Land Use Information System – NLUIS).

Mfumo huyo uliobuniwa na kutengenezwa na Tume, unatumika kukusanya taarifa za mmiliki, kupima, kuchakata na baadae kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila kieletroniki hali ambayo inawezesha kufanya mchakato wa uandaaji Hatimiliki za Kimila kutumia muda mfupi na kupunguza gharama.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Makete Mh. Festo Sanga, ameishukuru Serikali kwa fursa hiyo kwani ilikuwa ni ndoto kwa wananchi wa vijiji hivyo kupimiwa ardhi na kumilikishwa. “Hakuna mwananchi wa Kigala alikuwa na ndoto ya kumiliki ardhi, lakini kwa jitihada za Mh. Rais, leo wananchi wa Kigala wanaenda kuwa na hati za kimila ambazo zitawasaidia kwenye majukumu mbalimbali kwa ajili ya shughuli zao za kilimo”.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Bw. William Makufwe amewaasa wananchi kuiheshimu mipango ya matumizi ya ardhi waliojiwekea wao wenyewe ili iweze kuwasaidia kuepeuka migogoro kwani kila shughuli imepangiwa eneo lake.

“Mmewezeshwa, mmeelekezwa, mmeelimishwa na mkakubaliana nyinyi wenyewe kama Kijiji kwamba sehemu hii tufuge, kule tulime, tutunze misitu na vyanzo vya maji, sasa wito na rai yetu ni tuheshimu makubaliano haya mliojiwekea ili kuepusha migogoro” alisema Bw. Makufwe

Pia, Mkurugenzi Makufwe aliwataka wananchi hayo kutambua umuhimu wa zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha kwani lina lengo la kuwanaufaisha wao wenyewe kwenye shughuli zao za kiuchumi hasa za kilimo na ufugaji.

Kwa takribani wiki nne sasa wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imeweka kambi katika Wilaya ya Makete kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji pamoja upimaji wa mashamba kwa ajili ya utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila.

Mjumbe wa Kamati ya Usimamizi Matumizi ya Ardhi ya Kijiji (VLUM) akiwasilisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kijiji cha Kigala kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Antony Sanga

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (aliyesimama) akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kigala wakati wa Ziara ya kukagua kazi ya Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na umilikishaji ardhi Wilayani Makete

Mbunge wa Jimbo la Makete Mh. Festo Sanga akizungumza kwenye Mkutano wa Kijiji cha Kigala wakati wa Ziara ya Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kijiji humo.

Mpima Ardhi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Mikidadi Kalimng’asi akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi namna vifaa vya upimaji vilivyotumika kuhuisha mipaka ya vijiji wakati wa zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi Wilayani Makete

Mtaalamu wa TEHAMA kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Bw. Gerald Mseti (wa pili kulia) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi namna Mfumo wa Taarifa za Matumizi ya Ardhi (National Land Use Information System – NLUIS) unavyofanya kazi katika utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu, Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete pamoja na Wataalamu kutoka Tume na Halmashauri wanaowezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi na umilikishaji ardhi