Habari
DC Kiteto apongeza Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi Vijijini
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema, amepongeza kazi inayoendelea kufanywa na wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji Wilayani humo.
Akizungumza katika kikao kazi na wataalamu hao kupitia mtandao (online), DC Mwema amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya zoezi hilo, akibainisha kuwa kazi hiyo ni muhimu katika kuleta mpangilio mzuri wa matumizi ya ardhi na kuondoa migogoro isiyo ya lazima.
Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa uandaaji wa mipango hiyo unapaswa kufanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha hauzalishi migogoro mipya ya ardhi, bali unaleta suluhisho la kudumu kwa changamoto zilizokuwepo hapo awali.
“Ni muhimu sana kuhakikisha kuwa mnaposimamia zoezi hili, mnazingatia maamuzi ya wananchi na wakati huo huo kuwashauri kitaalamu ili kufikia maamuzi bora na yenye manufaa kwa jamii nzima,” amesema DC Mwema.
Aidha, amekemea vikali dhana ya ubaguzi miongoni mwa jamii za wakulima na wafugaji iliyoibuka katika baadhi ya Vijiji, akisisitiza uelimishaji na kuhakikisha kuwa mipango ya matumizi ya ardhi inapaswa kuzingatia usawa na haki kwa makundi yote ya wananchi bila upendeleo.
Katika kuongeza ufanisi wa zoezi hilo, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha kikamilifu Viongozi wa ngazi zote kuanzia Kata hadi Vijiji, ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa wa pamoja na usimamizi madhubuti wa mipango hiyo pindi itakapokamilika.
Pia ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa wataalamu hao na kuwa yuko tayari kupokea ushauri wa kitaalamu wakati wowote utakapohitajika, ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kama lilivyokusudiwa.
DC Mwema amewahimiza wataalamu hao kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa mipango ya matumizi ya ardhi, akieleza kuwa uelewa wa wananchi ni msingi muhimu wa utekelezaji wenye mafanikio.
Amesema licha ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa zoezi hilo, ana imani kuwa likifanyika kwa umakini na weledi, wataalamu hao wataweka historia katika Wilaya ya Kiteto kwa kuacha mfumo imara wa usimamizi wa ardhi.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, ataitisha kikao cha pamoja kitakachowahusisha Viongozi wa Halmashauri na Vijiji kwa lengo la kufanya tathmini na kujenga uelewa wa pamoja, ili mipango hiyo iweze kusimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi.
