Habari
Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi: Ufunguo wa Kutatua Changamoto za Matumizi ya Ardhi
Taasisi ya Kadasta (Land Registry and Mapping Agency), ambayo ni mhimili mkuu wa usimamizi wa taarifa za ardhi nchini Uholanzi, imebainisha kuwa upangaji matumizi ya, upimaji na umilikishaji wa ardhi ni miongoni mwa suluhisho muhimu katika kukabiliana na changamoto za matumizi ya ardhi.
Hayo yameelezwa wakati wa kikao kazi kati ya wataalamu wa taasisi hiyo na ujumbe kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), ulioambatana na wataalamu kutoka Benki ya CRDB, katika ziara ya kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na kiutendaji kati ya taasisi hizo pamoja na Chuo Kikuu cha Twente kupitia Kitivo cha ITC (Faculty of Geo-Information Science and Earth Observation).
Akitoa ufafanuzi kuhusu uzoefu wa Uholanzi, mtaalamu wa Kadasta, Christelle van de Berg, alisema kuwa nchi hiyo ilianza kupanga na kupima ardhi tangu miaka ya 1800, hali iliyowezesha kuwepo kwa mfumo imara wa ukusanyaji, uhifadhi na uhuishaji wa taarifa za matumizi ya ardhi na umiliki wake.
Alieleza kuwa kupitia mfumo huo, Kadaster husimamia kwa ufanisi mabadiliko ya matumizi ya ardhi na umiliki wake, jambo linalochangia kupunguza migogoro ya ardhi na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Vilevile, alibainisha kuwa Taasisi ya Kadasta ina jukumu la kukusanya na kusajili taarifa za kiutawala na kijiografia kuhusu mali na haki zinazohusiana na ardhi, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya matumizi ya ardhi na miundombinu ya takwimu za kijiografia (spatial data infrastructures), hali inayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na zilizojumuishwa katika sehemu moja.
Awali, ujumbe huo ulipata fursa ya kubadilishana uzoefu na wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Twente, ambapo Mkuu wa Idara ya Mipango (ITC), Profesa Karin Pfeffer, aliweka wazi fursa mbalimbali za kitaaluma zinazoweza kuwajengea uwezo wataalamu wa Tume katika maeneo ya upangaji wa matumizi ya ardhi, mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na usimamizi wa ardhi.
Aidha, wakufunzi wa chuo hicho waliwasilisha uzoefu wao katika uandaaji wa ramani (mapping), usimamizi wa ardhi (land administration) na utatuzi wa migogoro ya ardhi (land conflict resolution), ambazo ni nyenzo muhimu katika kuboresha upangaji endelevu wa matumizi ya ardhi.
Ujumbe huo unaongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Bw. Joseph C. Mafuru, na unahusisha pia wataalamu kutoka Benki ya CRDB, ambapo taasisi hizo zinatarajia kuimarisha ushirikiano katika masuala mbalimbali hususan yale yanayohusiana na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia mipango bora ya matumizi ya ardhi.
Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa, ikijumuisha mafunzo ya vitendo na mijadala ya kitaalamu itakayochangia kuimarisha uwezo wa taasisi katika kuwezesha Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
