Habari

Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuchochea mageuzi ya Kilimo

Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuchochea mageuzi ya Kilimo
Jan, 20 2026

Kuanza kwa zoezi la uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji limetajwa kuwa ni hatua muhimu inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo ikiwemo kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha elimu ya ugani, na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo kwa muda mrefu imekuwa kikwazo cha maendeleo Vijijini.

Zoezi hilo linalenga kupanga matumizi ya ardhi kwa utaratibu unaozingatia mahitaji halisi ya wananchi, kwa kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya kilimo, makazi, hifadhi ya mazingira, ufugaji na uwekezaji, ili kuhakikisha ardhi inatumika kwa tija na kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza katika Kijiji cha Pashungu, Mtaalamu wa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya amesema mipango hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha rasilimali ardhi inatumika kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Aliongeza kuwa mipango ya matumizi ya ardhi inapotekelezwa ipasavyo huondoa migogoro, huongeza uzalishaji, na kutoa mwelekeo wa wazi wa matumizi ya rasilimali, jambo linalochochea uwekezaji na kuimarisha ustawi wa jamii.

Aidha, mtaalamu huyo ameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo huenda ukavutia hata vijana kujihusisha na kilimo cha kisasa chenye mwelekeo wa kibiashara, kwani muda mrefu vijana wengi wamekuwa wakihama Vijijini kwenda Mijini kutokana na ukosefu wa fursa za ajira na uhakika wa kumiliki ardhi.

Sambamba na uandaaji wa mipango hiyo, maafisa ugani wameendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu mbinu bora za uzalishaji, matumizi sahihi ya pembejeo, pamoja na namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hatua hii inalenga kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula katika wilaya hiyo, huku ikichochea matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo.

Changamoto kubwa kwa wakulima wengi imekuwa ni ukosefu wa hati za umiliki wa ardhi, hali inayowazuia kupata mikopo katika Taasisi za kifedha. Kupitia mipango ya matumizi ya ardhi, wananchi watawezeshwa kupata Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs), hatua itakayowawezesha kutumia ardhi yao kama dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa mazao, ununuzi wa pembejeo, na ujenzi wa miundombinu ya kilimo.

Kwa ujumla, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi unaonekana kuwa hatua muhimu ya kuweka msingi wa uchumi wa Vijiji unaojitegemea. Endapo utekelezaji wake utaenda sambamba na elimu ya ugani, upatikanaji wa mitaji, na masoko ya uhakika, Wilaya ya Mbeya inaweza kuwa mfano wa kuigwa katika kutumia ardhi kama chombo cha maendeleo ya kilimo, ajira kwa vijana, na ustawi wa wananchi.