Habari
Maelekezo ya Rais Samia yaanza Kutekelezwa Katavi
Na WANMM, Mpimbwe, Katavi
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe. Geophrey Mizengo Pinda amekabidhi jumla ya Hati za Hakimiliki za kimila 691 kwa wanachi wa vijiji vya Ntilili na Igalukiro.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika tarehe 21 Novemba 2024 katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kasansa na kuhudhuriwa na wataalam wa Ardhi kutoka ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Katavi.
Naibu Waziri Pinda amesema kuwa hatua ya kukabidhi hati hizo ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupima ardhi ya nchi nzima.
"Hizi zote ni juhudi za Mama Samia Suluhu Hassan, anataka nchi nzima hii ipimwe, watu wake wawe na hivi vibali vya ardhi yao" amesema Naibu Waziri Pinda.
Mhe. Pinda amesema kuwa vijiji vya Ntilili na Igalukiro vimenufaika na uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyowezeshwa kuandaliwa Hatimiliki 691 kupitia ufadhili wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
"Kupita mradi huu, Ofisi ya Makamu wa Rais imetufadhili tupime vijiji vinavoambatana na Mradi wake hapa juu (Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Uhifadhi wa Banowai) kwa hiyo wanufaika ni Ntilili na Igalukiro ambapo tumeyarisha hati 691 zote zipo hapa" ameongeza Mhe Pinda.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Katavi ndg Chediel Mrutu amewaasa wanakijiji hao kuhifadhi hati hizo sehemu salama kwani zikiharibika si rahisi kupata nakala mbadala.
"Hizi hati ukiweka kwenye eneo ambalo linavuja itaharibika na ikiharibika siyo rahisi kupata nakala yake"
"Zamani watu walikuwa wanafanya lamination, hii hairuhusiwi, tafuta kibegi chako kizuri na salama iweke na itunze" amesema Kamishna Mrutu.
Naye Afisa Mipangomiji Mkoa wa Katavi ndugu Flavian Masore wakati akisoma taarifa ya mpango wa matumizi bora ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe amesema mpango huo umewezesha kutoa elimu ya ardhi na kutenga maeneo muhimu kwa ajili ya matumizi ya bora ya ardhi pamoja na kuandaa hati za ardhi.
"Vijiji vimewezeshwa kutenga maeneo ya matumizi mbalimbali ya kilimo, makazi vyanzo vya maji hifadhi za misitu maeneo ya malisho pamoja na kutunga sheria ndogo za usimamizi wa maeneo hayo”