Habari

Mafuru ataka Uwajibikaji wenye kuleta Matokeo Chanya

Mafuru ataka Uwajibikaji wenye kuleta Matokeo Chanya
Sep, 17 2024

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Bw. Joseph C. Mafuru amewaasa watumishi wa Tume hiyo kuwajibika ipasavyo katika kutimiza jukumu yao ili kuleta matokeo chanya yatakayosaidia kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa kazi za Tume katika nyanja mbalimbali na kusukuma jitihada za maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mafuru ameyasema hayo kwenye Kikao Kazi kati yake na Watumishi wa Tume hiyo kilichofanyika tarehe 13/09/2024, Makao Makuu ya Ofisi za Tume zilizopo Jijini Dodoma. Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kupata maoni kutoka kwa watumishi na kuweka mipango “road map” itakayosaidia katika utekelezaji wa kazi za Tume chini ya uongozi wake.

Aidha, Bw. Mafuru aliwataka Watumishi kufanya kazi kwa kushirikiana baina yao pamoja na wadau mbalimbali huku wakifuata Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu zilizopo ili kuondokana na mapungufu yanayoweza kusababisha kudhorotesha ufanisi wa kazi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mafuru ameagiza kuimarishwa na kuwezesha ofisi za Kanda zilizopo katika Mikoa mbalimbali nchini, ili Ofisi hizo ziweze kutekeleza majukumu ya Tume ipasavyo na kutimiza lengo la kuanzishwa kwa ofisi hizo likiwemo kusogeza huduma kwa wananchi na wadau wengine.