Habari
Mafuru afunga Mkutano Mkuu Wa Wataalamu wa Mipango Miji
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Bw. Joseph C. Mafuru, amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga kufunga Mkutano Mkuu wa 10 wa Mwaka wa Wataalamu wa Mipango Miji (AGM-10) uliofanyika tarehe 27 - 28 Novemba 2025 Jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano huo, Bw. Mafuru aliwataka wataalamu wa Mipango Miji na Vijiji kuongeza bidii na kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na uadilifu ili kukidhi matakwa ya jamii na kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa inatekelezeka. Alisisitiza kwamba taaluma ya upangaji wa ardhi inahitaji watu wanaojiongeza kila mara, wanaotafuta maarifa mapya na wanaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya kijamii.
Vilevile, aliwahimiza wataalamu hao kujitambulisha kwa kazi zao na kuwa nguzo muhimu katika Taasisi wanazofanyia kazi kwa kuzingatia maadili, kufanya kazi kwa kushirikiana, na kuhakikisha mipango inayotengenezwa inaendana na Sera, Sheria na Miongozo ya Kitaifa kuhusu matumizi ya ardhi.
Mkutano wa 10 wa mwaka wa Wataalamu wa Mipango Miji na Vijiji uliwaleta pamoja wataalamu hao ili kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kujenga mikakati ya kuboresha Upangaji na Usimamizi wa ardhi kwa maendeleo endelevu ya Miji na Vijiji nchini.
