Habari
Mafuru: Ushirikishwaji wa Wadau ni Muhimu katika Kulinda Mazingira
Na: Sidi Mgumia, Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bw. Joseph Mafuru amesema ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kulinda mazingira na kutekeleza kwa urahisi mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
Bw. Mafuru ameyasema hayo alipokuwa akiongea na waandishi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), wanaotekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), waliotembelea Ofisi za Tume mjini Dodoma hivi karibuni.
Mkurugenzi Mafuru ameeleza kuwa wadau hao ambao ni wa uhifadhi, wananchi, Taasisi za wanyamapori na wengineo wanapaswa kushirikishwa katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kisha kusimamia kwa pamoja ili kurahisha utekelezaji wake.
“Ili uweze kuwashirkisha wadau, inafaa kuanza kuandaa mipango ya ardhi kwa pamoja na kisha mkaisimamia kwa pamoja hivyo kuitekeleza inakuwa ni rahisi sana. Lakini usipowashirikisha utekelezaji wake utakuwa mgumu sana, kwa hivyo kuna haja ya wadau wote kushiriki kwa pamoja kuhakikisha zoezi hilo linafanyika vilivyo,” alisema Bw. Mafuru.
Aidha, Bw. Mafuru alisema kuwa kama Tume wanapambana kupata wadau wakutosha ili kuhakikisha wanaongeza kasi ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi nchini. Kwa sasa, Vijiji vilivyoandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi bado ni vichache, kwani hadi kufikia Julai 2024, takribani Vijiji 3000 vimeandaliwa Mipango hiyo kati ya vijiji 13,000 ambapo ni ishara kuwa bado kuna kazi kubwa yakufanya.
“Tukiongozwa na Serikali ikifuatiwa na wadau wengine kwenye masuala ya uhifadhi mazingira na wanyamapori, tunapaswa tuhakikishe tunaandaa mipango yakutosha. Kwani kadri tunavyozidi kuchelewa kupanga maana yake tunaendelea kutengeneza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, hivyo ni heri tukaifanya mapema hiyo mipango ili kuepusha hiyo migogoro,” alisema Bw. Mafuru.
Mkurugenzi Mafuru alieleza kuwa, ili kukabiliana na kasi ya upangaji matumizi ya ardhi nchini, Serikali imeendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya kazi hiyo, na kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025, zaidi ya shilingi bilioni tano zimetengwa kwa ajili yakuhakikisha Vijiji vingi zaidi vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
Akizungumzia juu ya mafanikio ya kuwepo kwa mipango ya matumizi ya ardhi, Mkurugenzi wa Utafiti, Uzingatiaji na Taarifa za Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Joseph Paul amesema kuwa mipango ya matumizi ya ardhi imesaidia wanakijiji kutokuingia maeneo ya hifadhi lakini pia imesaidia kuokoa mapito ya wanyama na kuwafanya wapite kama ambavyo wanapaswa kupita.
Kimsingi tunafahamu wanyama kama tembo huwa hawasahau njia zao, kwa kupitia Serikali za Vijiji lakini pia wazee ambao wana uzoefu na maeneo hayo wamesaidia kuainisha maeneo ambayo yana umuhimu wa uhifadhi na kuyatenga kwa matumizi rafiki ambayo hayatazuia wanyama kupita lakini shughuli za kibinadamu kuendelea,” alisema Dkt. Paul.
Dkt. Paul, aliendelea kusema kimsingi Tume ya Taifa ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi imeratibu na kusaidia uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya Kanda, Mkoa, kwa mfano ukanda ambao ni muhimu kwa uhifadhi kama Mkoa wa Mara, mpango umeendelea kuandaliwa ili kuhakikisha kunakuwa na matumizi sahihi ya ardhi.
“Lakini pia tumegundua kwenye tafiti zetu kwamba ili tusaidie kusiwe na muingiliano wa kimatumizi kuna umuhimu wakuboresha maisha ya wananchi wenye maeneo yao. Moja ya njia za kuboresha ni kuhakikisha kwamba wana uhakika wa umiliki wa ardhi, kwa hivyo Tume imewezesha uandaaji hati miliki za kimila zaidi ya 20,000 kwa maeneo yenye umuhimu wa uhifadhi.”
“Wanakijiji wa maeneo hayo wamepewa hati miliki za kimila kwa kuzingatia vigezo mbalimbali pamoja na kuhakikisha kuwa jinsia katika umiliki inazingatiwa, kwenye familia tumehakikisha mume na mke wanamilikishwa yale maeneo yao pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa ndani na nje ili kusaidia wananchi kutumia maeneo yao vizuri kwa kilimo na ufugaji wenye tija,” alisema Dkt. Paul.
Pamoja na hilo, Paul alisema kuwa ukosefu wa elimu ya matumizi bora ya ardhi bado ni changamoto kwa wanajamii, hivyo bado wanaendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa utunzaji na umuhimu wa utekelezaji mpango wa matumizi ya ardhi.
Kwa upande wake Afisa Ardhi Mkuu wa Tume, Bw. Nyerembe Munasa alisema ili kuwe na maendeleo endelevu wanapendekeza kuwe na mipango ya matumizi ya ardhi katika Mikoa yote nchi nzima, na Kanda zilizopo mfano ikolojia ya Ziwa Victoria, Tanganyika, Serengeti na kwingineko, inahitajika kuhifadhi maeneo ya ikolojia kwa kuzingatia matumizi ya ardhi katika ngazi za Mikoa.
“Kuna umuhimu mkubwa sana kulinda mifumo ya ikolojia, lakini nchi yetu ina mifumo mingi ya ikolojia ambayo hailindwi hasa hizi shoroba ambazo wanyama hutumia kutoka kwenye hifadhi moja kwenda nyingine. Kwa bahati mbaya unakuta miongoni mwa hizi shoroba nyingi zimezibwa kwa aidha shughuli za kilimo au makazi ya binadamu jambo linalosababisha migongano kati ya wanyama na binadamu.”
“Hakukuwa na mikakati au mipango ambayo ilikuwa inaelekeza namna gani hayo maeneo yahifadhiwe. Lazima tufanye uongozaji wa hizi shoroba kwa kutumia mipango Shirikishi ya Matumizi ya Ardhi, ili kuwe na maendeleo endelevu sababu yana umuhimu wake kiuchumi, kijamii na pia katika mambo ya mazingira na kiikolojia,” alisema Bw. Munasa.
Vilevile, Bw. Munasa aliongeza kuwa, “Kuhusu shoroba ziko 66 lakini ni mbili tu ndizo zimefanyiwa kazi ikiwemo shoroba ya Ifakara. Changamoto kubwa iliyokwamisha zoezi hili ni fedha na hii ni kwa sababu shoroba ziko nyingi na tunahitaji kuwa na mipango ya matumizi katika Vijiji vyote vinavyopitiwa na shoroba.”
Naye Mkurugenzi Msaidizi Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa ameongeza kuwa kama hakuna usimamizi mzuri hizo shoroba hazitakuwepo, mipango itapangwa lakini hazitakuwepo, kwa hiyo ni vyema kuangalia namna ya kuwashirikisha wananchi wakati mipango inaandaliwa kwa sababu wao ndio wahusika wakuu katika suala zima la kuwepo ama kutokuwepo kwa shoroba hizo.
“Tume ina wajibu wa kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa kwa ngazi zote inasimamiwa kama ilivyopangwa. Muhimu kwa wanajamii, wataalamu na wadau wengineo kushirikiana juu ya masuala ya ardhi,” alisema Kishoa
Hata hivyo, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo ameongeza kuwa katika mapambano dhidi ya changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, elimu ya mazingira na haswa uhifadhi bado inahitajika ipelekwe kwenye jamii lakini pia kusisitiza uwepo wa ushirikishwaji wa sekta na Wizara mbalimbali katika masuala ya mazingira.
“Ikiwa wadau muhimu kama vile Wizara ya Maliasili na Utalii, watunga Sera, waandishi wa habari na wengineo watashirikiana kwa pamoja katika maandalizi ya sera, mipango na michakato ya usimamizi wa mazingira itasaidia kulinda, kuhifadhi, kutunza na kusimamia mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadae,” alisema Chikomo