Habari

Makamu wa Rais akabidhi Hati Miliki za Kimila Makete

Makamu wa Rais akabidhi Hati Miliki za Kimila Makete
Oct, 27 2023

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 27/10/2023 amekabidhi Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi wa Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kijiji cha Tandala Wilayani humo.

Akizungumza mbele ya Makamu wa Rais, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amesema kuwa utolewaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila unafuatia uwezeshaji wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji uliofanywa na Wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC).

Kwa mujibu wa Mhe. Pinda Mkoa wa Njombe una jumla ya Vijiji 323 na kati ya hivyo, Vijiji 295 tayari vimewezeshwa kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na bado kuna mikakati inaendelea kufanyika ili kuhakikisha Vijiji vyote katika Mkoa huo vinafikiwa.

“Mh. Makamu wa Rais, Mkoa wa Njombe tunavyo Vijiji 323 na kati ya hivyo Vijiji 295 tayari vimewezeshwa (kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi) na sasa tuko kwenye Wilaya hii ya Makete kama taarifa ilivyosema, unakwenda kukabidhi hati chache kwa niaba ya wengine, na bado tunaendelea na mkakati wa kukamilisha Mkoa mzima baada ya muda kidogo” alisema Mhe. Pinda

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Bw. William Makufwe amesema kuwa upatikanaji wa Hatimiliki hizo ni jitihada za Wilaya katika kukuza kilimo cha zao la ngano linalozalishwa kwa wingi katika Wilaya hiyo.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, Wilaya yake imeamua kuendesha kilimo cha zao hilo Kimkakati na kwa kushirikiana na Tume, wamewezesha upangaji wa matumizi ya ardhi ya Vijiji, kupima na kumilikisha mashamba ya wananchi kupitia Hati za Hakimiliki za Kimila ili ziwape fursa wananchi kuongeza mitaji ambayo itatanua wigo wa uzalishaji wa zao hilo.

Ugawaji wa Hatimiliki hizo unafuatia kazi iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Makete ambapo imewezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 64 na kutoa jumla ya Hatimiliki za Kimila 6,883

Kazi hiyo imetekelezwa katika awamu mbili ambapo, awamu ya kwanza, ilihusisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 44 na upimaji wa vipande vya ardhi katika vijiji 17 ambapo jumla ya hati 6,594 ziliandaliwa.

Aidha, awamu ya pili ilihusisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 20 kwenye Tarafa za Ukwama na Lupalilo ambapo Vijiji 20 viliwezeshwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na Hati za Hakimiliki za kimila 289.

Kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, na Miongozo, Hati za Hakimiliki za Kimila hutolewa katika ardhi za Vijijini pindi Vijiji hivyo vinapokuwa vimekamilisha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa mujibu ya mahitaji yao.

Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe, Pili Msati, Meneja wa Tume Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Edward Mwaigombe, Afisa Ardhi (W) Makete, Obed Katonge, Mkurugenzi Msaidizi Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Fulgence Kanuti, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Njombe wakiwa tayari kumpokea Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe (kushoto) akitoa maelezo kwa Makamu wa Rais Mhe. Philip Mpango juu ya kazi ya uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi na utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila.


Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua moja ya taarifa ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Kijiji cha Bulongwa, Wilayani Makete kabla ya kukabidhi Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi Wilayani humo

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhi Hati ya Hakimiliki ya Kimila kwa mwananchi aliyepimiwa na kumilikishwa ardhi katika kata ya Lupalilo Wilayani Makete


Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango akiteta jambo na mwananchi kabla ya kumkabidhi Hati yake


Baadhi ya wananchi kutoka kwenye Vijiji mbalimbali Wilayani Makete wakimiminika kuchukua Hati zao


Wananchi kutoka Vijiji mbalimbali Wilayani Makete wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kukabidhiwa Hati zao