Habari

Mamlaka za Upangaji Matumizi ya Ardhi Zapatiwa Mafunzo

Mamlaka za Upangaji Matumizi ya Ardhi Zapatiwa Mafunzo
Oct, 30 2021

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeanza mkakati wa kuzijengea uwezo Halmashauri za Wilaya ambapo kwa kushirikiana na Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP-2) imeendesha mafunzo ya kujengea uwezo wataalamu kutoka Halmashauri 4 za Wang’ing’ombe, Njombe, Ludewa na Mufindi ili kuweza kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa mujibu wa vigezo na viwango vilivyoainishwa kwenye Sheria na Mwongozo wa Upangaji Matumizi ya Ardhi nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Tume, anayeshughulikia Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi, Bw. Dioscory Kanuthi, amesema kuwa uwepo wa mafunzo hayo ni utekelezaji wa moja la jukumu la msingi la Tume lililowekwa kisheria na miongozo mbalimbali pamoja na maagizo ya viongozi wa Serikali.

“Ukisoma ile Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, imeeleza kuwa moja la jukumu la Tume ni kujengea uwezo Halmashauri za Wilaya na kushuka chini hadi kwenye Halmashauri za Vijiji, lakini pia uendeshaji wa mafunzo haya ni utekelezaji wa Ilani ambapo hadi kufikia 2025 inatakiwa tuwe tumewajengea uwezo Halmashauri 83 kote nchini”, alisema Bw. Kanuthi.

Aidha, Meneja wa Tume Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bibi Pili Msati amesema kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka kwani hivi karibuni wanatarajia kuanza zoezi la kuwezesha kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji zaidi ya 40 katika ukanda huo, hivyo kwa kuwajengea uwezo wataalamu hao, itafanya kazi hiyo kufanyika kwa haraka na viwango.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Bw. Jeswald Ubisimbali ameishukuru Tume kwa kuwaletea mafunzo hayo kwani yamewafungua kwa sehemu kubwa na kuanzia sasa watafanya kazi kwa weledi kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na Tume.

Kwa upande wake, Mtaalamu kutoka Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP-2) Bw. Andrew Ferdinands amesema kuwa moja ya shughuli katika programu hiyo ni kuviwezesha vijiji vya mradi vilivyopo kwenye Wilaya hizo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kuyasimamia na kuainisha njia za kuzuia moto katika maeneo ya misitu ya kupandwa yaliyotengwa.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Njombe, yamewakutanisha wataalamu zaidi ya 40 wanaounda timu za Uandaaji na Usimamizi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (PLUM Teams) ambazo zinajumuisha sekta mtambuka zinazohusiana na rasilimali ardhi zikiwemo Kilimo, Mifugo, Misitu, Wanyamapori, Maji, Sheria, mazingira, Maendeleo ya Jamii na wataalamu wa GIS kutoka katika Wilaya hizo.