Habari
Mara yaandaliwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Mkoa na Kanda
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imekamilisha kazi ya uandaaji Mpango ya Matumizi ya Ardhi ya Mkoa wa Mara na Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kanda unaojumuisha Wilaya za Bunda na Musoma zilizopo kwenye ukanda wa chini wa Mkoa huo.
Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Mkoa wa Mara (Mara Regional Land Use Framework Plan) umelenga katika kutambua fursa mbalimbali za rasilimali ardhi zilizopo katika Mkoa wa Mara na kuzipangia namna zinavyoweza kutumika ili kuchochea shughuli za maendeleo za Mkoa huo.
Aidha, katika Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa sehemu ya Ukanda wa Chini mkoani Mara, ambao unajumuisha Wilaya za Bunda na Musoma (Musoma – Bunda Lowland Zone Land Use Framework Plan) umelenga katika kuibua uwezo wa Wilaya hizo kutumia rasilimali zilizopo katika ukanda wa chini mkoani humo, hususani Ziwa Victoria ili kuinua uchumi kutokana na shughuli kuu zinazofanyika katika maeneo hayo.
Rasimu za Mipango hiyo imewasilishwa kwenye Kikao cha Wadau wa Matumizi ya Ardhi mkoani Mara kilichofanyika tarehe 20/09/2024 ili kupata maoni kutoka kwa wadau hao na kufanya maboresho kabla ya kuiwasilisha kwa hatua za uidhinishaji na kuanza utekelezaji wake.
Akifungua Kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Dominicus C. Lusas amesema kuwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ngazi ya Mkoa na Kanda imebainisha fursa zilizopo na kutoa mwongozo wa Matumizi ya rasilimali Ardhi Mkoani humo ili kuwa na maendeleo endelevu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kimazingira.
“Fursa zilizopo kwa mkoa wa Mara hususani katika uzalishaji wa kilimo na Mifugo inachagiza mipango hii iwezeshe kuchochea ufufuaji na uanzishaji viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo na Mifugo, kukuza sekta ya Utalii, Madini na kuleta maendeleo kupitia Uchumi wa buluu” alisema Bw. Lusas.
Vilevile, Bw. Lusas alieleza kuwa kukamilika kwa Mipango hiyo kutasaidia watumiaji mbalimbali wa Ardhi, wataalamu katika Taasisi mbalimbali, waandaaji wa mipango ya maendeleo, viongozi, Wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuweza kutambua Matumizi yanayofaa kwa kila kipande cha Ardhi kwa ukubwa, ubora na uwezo wa Ardhi iliyopo katika Mkoa wa Mara.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kikanda, Mikoa, Wilaya na Vijiji (ZORED) Bw. Nyerembe Munasa ambaye pia alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tume amesema kuwa uandaaji Mipango hiyo ni mhimili muhimu wa uendelezaji wa matumizi ya rasilimali za ardhi kwa uwiano unaofaa katika ngazi ya Mkoa na Kanda.
“Mipango hii ni muhimu katika maendeleo ya Mkoa, hivyo kupitia mkutano huu tunategemea michango yenu ya mawazo itakayotoa dira ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Mara na Kanda kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na uwekezaji kwa kipindi cha miaka 20 ijayo” alisistiza Bw. Munasa
Aidha, Bw. Munasa alifafanua kuwa Mpango wa Kanda ulioandaliwa umelenga kuibua fursa za uchumi wa buluu zinazopatikana katika Ziwa Victoria hususan ukanda wa chini wa Mkoa wa Mara katika Wilaya za Bunda na Musoma kama ulivyofafanuliwa katika Mpango Mkakati wa Mkoa wa Mara.
Mipango hiyo imeandaliwa na wataalamu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri zote 9 zilizopo katika Mkoa wa Mara.
Kazi hizo zimetekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Sura 116 chini ya Mradi wa Uandaaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kikanda, Mikoa, Wilaya na Vijiji (ZORED) unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea na Afrika (KOAFEC) kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).