Habari

Mashamba na Makazi yapo ya Kutosha Msomera, Wananchi wapokea Hati za Hakimiliki za Kimila

Mashamba na Makazi yapo ya Kutosha Msomera, Wananchi wapokea Hati za Hakimiliki za Kimila
Sep, 20 2024

Na Eleuteri Mangi, Handeni

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekabidhi Hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi waliohamia Msomera kwa hiari wakitokea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya makazi na mashamba ili kuendelea na shughuli zao za kila siku za kijamii na kiuchumi.

Akikabidhi Hati za Hakimiliki kwa wananchi hao Septemba 19, 2024 eneo la Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amesema mashamba na makazi kwa wananchi wa msomera yapo ya kutosha.

Waziri Ndejembi amesema Serikali inatekeleza mradi wa kujenga nyumba na kuwapatia mashamba wananchi wanaohama kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda vijiji vya Msomera, Lengusero, Saunyi na Kitwai ‘B’ vilivyopo katika mkoa wa Tanga na kusisitiza maeneo yote yapangwe na kupimwa kwa ajili ya makazi na mashamba.

“Hakikisheni mnapomilikishwa makazi na mashamba, wekeni alama ili mjue mashamba yenu yapo wapi. Serikali imewapa haya maeneo ni ya kwenu, wajibu wa kuyalinda na kuyatunza ni wa kwenu ninyi. Yatunzeni maeneo haya yatumike kwa vizazi na vizazi” amesema Waziri Ndejembi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Dkt. Batilda Buriani amewahimiza wananchi wa Msomera kujiandikisha na kupata Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambayo vitawarahisishia kupata Hati Miliki za maeneo yao kwa kila familia ikiwahusisha waume pamoja na wake zao hatua inayomaliza malalamiko ndani ya familia.

Akitoa taarifa ya hati ambazo tayari zimetolewa, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema zoezi la utoaji Hati za Hakimiliki ya Kimila katika eneo la Msomera ni endelevu ili kuhakikisha wananchi wote waliohamia eneo hilo pamoja na wenyeji wanamilikishwa maeneo ambayo yamepangwa na kupimwa.

Mhandisi Sanga amesema zoezi hilo limefanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilitolewa Hati 1142 zikijumuisha nyumba 503, mashamba 500 pamoja na Hati 139 za wenyeji ambao tangu awali walikuwa wakiishi katika eneo hilo.

Katika awamu ya pili zimetolewa jumla ya hati 1674 kwa ajili ya makazi na mashamba na tayari ipo Mipango kina ya Makazi nane ambayo ina viwanja vya makazi na huduma za jamii 7,253 sawa na asilimia 145 ya lengo la viwanja 5,000 lililowekwa, mashamba 9,807 sawa na asilimia 123 ya lengo la mashamba 8,000 yamepimwa na kufanya jumla ya viwanja na mashamba yaliyopimwa kuwa 17,060.

Aidha, matumizi mengine yaliyopangwa na kupimwa katika eneo hilo ni pamoja na viwanja vya uwekezaji, shule, zahanati, vituo vya Afya, stendi, maeneo ya wazi, misikiti, makanisa, vituo vya polisi, mashamba darasa, majosho, machinjio, makaburi na miundombinu ya barabara pamoja na hekta 84,940.8 kwa ajili ya malisho.

Kwa upande wao wananchi wa Msomera Bw. Oloitu Oseitai na Bi. Elizabert Laizer wamesema eneo hilo limepangwa vizuri wanafurahia maisha kwa kuwa wanapata mahitaji yote ya msingi anayopaswa kupata mwanadamu ikiwemo huduma za afya, elimu, barabara na mahitaji mengine pia wana uhuru wa kufanyakazi za kilimo, ufugaji na biashara tofauti na hapo awali walipokuwa Ngorongoro.