Habari

Mgogoro wa mpaka Vijiji vya Tumbi na Ngehe wapata Mwarobaini

Mgogoro wa mpaka Vijiji vya Tumbi na Ngehe wapata Mwarobaini
Oct, 28 2024

Na Halima Salum, Mbamba-bay, Nyasa

Wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Ruvuma pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa wamefanikiwa kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Tumbi na Ngehe uliodumu kwa takribani miaka 14.

Mgogoro huo uliotokana na mgawanyiko wa Vijiji hivyo, ambapo hapo awali, Kijiji cha Ngehe kilikuwa ni Kitongoji ndani ya Kijiji cha Tumbi, na baada ya kutokea mgawanyiko, wananchi hawakuonyeshwa mipaka halisi ya kiutawala ya Vijiji hivyo hali iliyopelekea kuwa na mvutano wa muda mrefu juu ya sehemu halisi Vijiji hivyo vinapopakana.

Wakizungumza mara baada ya kukutanishwa, kufanya majadiliano na kupata muafaka juu ya mpaka huo, baadhi ya Viongozi na wananchi wa Vijiji hivyo wameishukuru Serikali kwa kuingilia kati mgogoro huo, kuwafanya wakubaliane na kuweka alama za kudumu za mpaka huo.

“Mgogoro huu ulikuwa unatusababishia wananchi kuvutana hasa linapokuja suala la kilimo na ufugaji, kila mmoja anavutia upande wake, ila kwa sasa kwa kuwa tumekubaliana na kuweka alama za kudumu za mpaka huu, tunaishukuru Serikali kwa kufanya hivi, kwa kuwa sasa hatutavutana tena” alisema Bw. Gidion Chindengwike, Mwenyekiti wa Kijiji cha Tumbi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngahe Bw. Eliud Ndiu amekiri kuwa, sintofahamu ya wapi ulipo mpaka huo ilikuwa ni changamoto wakati akitekeleza majukumu yake, ila baada ya makubaliano hayo anaamini changamoto hiyo itakuwa imepatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Hakukuwa na utambuzi wa mipaka halisi ya kiutawala baada ya kugawanywa kutoka kwenye Kijiji mama cha Tumbi, kila mara ilitupekea kuwa na mvutano na wenzetu, lakini kupitia zoezi hili lililofanyika tunashukuru hakutakua tena na changamoto hiyo ya kutofautiana kutokana na mipaka imeonyeshwa na tumekubaliana na wataalamu wamechukua vipimo na kupanda mawe” alisisitiza Bw. Ndiu

Naye Hilda Chilo mkazi wa Kijiji cha Tumbi amepongeza ujio wa zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi kwani kwa sehemu kubwa limewasaidia jamii yao kuwa na uelewa mpana juu ya masuala ya ardhi Kijijini hapo pamoja na kuwa suluhisho la baadhi ya masuala ya matumizi ya ardhi yaliyokuwa hayaendi sawa.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu tumepata elimu ya masuala ya ardhi ambayo itatusaidia haswa kwenye utatuzi wa migogoro ya ndani kutokana na kwa sasa tumeunda Baraza la Ardhi, pia itatusaidia kuondokana na matumizi holela ya ardhi na utunzaji wa mazingira hasa vyanzo vya maji baada ya kutenga maeneo ya vyanzo vya maji na kuyatungia Sheria ya kuyasimamia” alisema Bi. Chilo

Akitoa ufafanuzi mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo lililopekelea kumalizika kwa mgogoro huo, Mpima Ardhi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Bw. Hamisi Hamdu ameeleza kuwa kudumu kwa muda mrefu kwa mgogoro wa mpaka huo kwa kiasi kikubwa pia umechangiwa na Viongozi wa Vijiji hivyo kukosa uelewa juu ya usimamizi wa ardhi za Vijiji vyao.

“Kwa kiasi kikubwa, elimu ya usimamizi wa ardhi imekuwa changamoto hapa, maana walikuwa wanagombana pindi wananchi wa Kijiji kimoja, wakifanya shughuli kuvuka Kijiji kingine, sasa baada ya kukubaliana na kupima mpaka huu, tumewapa pia elimu ya kutosha kuhusu mipaka ya kiutawala kutokuwa kikwazo cha kufanyika kwa baadhi ya shughuli hadi kwenye Kijiji kingine” alisisitiza Bw. Hamdu.

Aidha, Bw. Hamdu aliongeza kuwa pindi Vijiji vikigawanyika na kukaa muda mrefu bila kupima upya mpaka unaotenganisha Vijiji hivyo, hutokea sintofahamu zinazopelekea kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri hiyo ya Nyasa.

Vilevile, Mpima huyo wa Halmashauri alieleza kuwa ujio wa zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi imewezesha kutatua mgogoro mwingine wa mpaka kati ya Vijiji vya Mkili na Ng’umbo, Ndonga na Kihagala pamoja na uhakiki wa mipaka ya Vijiji vingine 8 uliopelekea marekebisho ya ramani za upimaji ili kuendana na uhalisia.

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imekamilisha kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji 14 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa huku ikifanikiwa kutoa elimu kwa wananchi, kuhuisha baadhi ya mipaka ya Vijiji iliyokuwa na shida pamoja na kuwawezesha wananchi wa Vijiji hivyo kutunga Sheria Ndogo za usimamizi wa mipango hiyo.