Habari
Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kuimarisha Mazingira na Usalama wa Chakula Katika Vijiji 17

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira imeanza kazi ya kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 17 vinavyokabiliwa na tishio la upungufu wa chakula kutokana na uharibifu wa mazingira uliopelekea hali ya nusu jangwa katika Wilaya nne za Kondoa, Magu, Nzega na Mkalama.
Kazi hiyo inayotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha takribani miezi mitatu kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2019 imetanguliwa na utoaji wa elimu kwa wananchi wa vijiji husika juu ya masuala mbalimbali yanayohusu ardhi kama vile maliasili, mazingira, kilimo na ufugaji.
Elimu hii inatarajiwa kuwasaidia wananchi kuendesha shughuli hizo kwa ufanisi ili kuwa na uzalishaji wenye tija wa mazao ya kilimo na mifugo. Aidha, mara baada ya kukamilika kwa upangaji wa matumizi ya ardhi, wakazi wa vijiji 6 vilivyopo katika Wilaya hizo nne watanufaika na zoezi la kupima mashamba na kutoa hati milki za kimila 300 kwa kila kijiji. Utoaji wa hati hizi za kimila utakuwa wa mfano na unatarajiwa kusaidia kuimarisha milki za maeneo kwa baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wakiwemo wanawake, vijana na wazee.
Akizungumzia juu ya utekelezaji wa kazi hiyo, Mtaalamu wa Masuala ya Mazingira kutoka Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi Bi. Suzana Mapunda, amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira, kuna hatari kubwa hapo baadae wananchi wa baadhi ya maeneo kukosa chakula endapo watashindwa kutumia ardhi vizuri.
“Tunakwenda kujenga uwezo na kuwezesha upangaji wa matumizi ya ardhi kwenye vijiji ambavyo vina upungufu wa chakula ili kukuza lishe kwa wananchi wa maeneo hayo. Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi utawezesha uboreshaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na malisho ya mifugo katika maeneo hayo. Tunalenga pia katika utunzaji wa mazingira ili kufanya matumizi ya ardhi yaliyo endelevu kwani mara tu baada ya kutengwa kwa maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali ni rahisi kufanya usimamizi wa matumizi ya ardhi hiyo” Alisema Bibi Mapunda.
Bi Mapunda alisisitiza na kutoa mifano ya namna usimamizi wa matumizi ya ardhi utakavyofanyika katika vijiji hivyo. Alisema maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya misitu ya hifadhi yatatunzwa kupitia Kamati za Mazingira za Vijiji ambapo shughuli rafiki na uhifadhi ndizio zitaruhusiwa kwa utaratibu utakaowekwa.
Vile vile, maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya kilimo na mifugo yatasimamiwa na wanavijiji kwa msaada wa wataalamu wa sekta husika ambao watawafundisha wanavijiji mbinu bora za kilimo na ufugaji ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa bora.
Kazi hiyo inafanyika katika vijiji vya Haubi, Mafai, Ntomoko, na Mwisanga katika Wilaya ya Kondoa, pamoja na vijiji vya Lumeji, Iseni, na Nyanghanga vilivyopo katika Wilaya ya Magu. Vijiji vingine vitakavyonufaika na maradi huo ni pamoja na Nyamlangwa, Bulende, Iboja, Bulambuka na Sigili vilivyopo katika Wilaya ya Nzega, na vijiji vya Mkiko, Mpambala, Nyahaa, Lugongo na Munuli vya Wilaya ya Mkalama.