Habari

Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 46 Pembezoni mwa Hifadhi za Taifa za Wanyamapori Yakamilika

Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 46 Pembezoni mwa Hifadhi za Taifa za Wanyamapori Yakamilika
May, 02 2019

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) pamoja na Halmashauri za Wilaya Karatu, Simanjiro, Kondoa, Bariadi na Bunda imekamilisha uwezeshaji wa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 46 kati ya 95 vya awamu ya kwanza vilivyopo pembezoni mwa hifadhi za Taifa za wanyamapori.

Kazi hiyo inalenga kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji jirani na hifadhi ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara na imeambatana na utoaji elimu ya uhifadhi, usimamizi wa rasilimali ardhi, mazingira pamoja na sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi nchini.

Akizungumzia hatua hiyo, Mratibu wa mradi huo kutoka Tume Rose Mdendemi amesema kuwa pamoja na kuanza nyuma ya muda na kukutana na changamoto za migogoro ya mipaka, kazi hiyo kwa ujumla inaendelea vizuri na sasa ipo kwenye hatua nzuri ya kufikia lengo lililowekwa ifikapo Juni 30.

“Mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na wanaona zoezi hili limechelewa kuwafikia hali iliyopelekea kuishi na migogoro mingi ya ardhi.” Alisisitiza Bibi Mdendemi na kuongeza “Katika Wilaya zote ambazo tumeanza nazo, vijiji vingi vilikuwa na migogoro, ila kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali za utatuzi wa migogoro zinazotajwa kwenye sheria, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua migogoro hiyo na wananchi wa vijiji hivyo wameendelea na kazi ya kupanga mipango ya matumizi ya ardhi.”

Aidha bibi Mdendemi amefafanua kuwa, migogoro mingi wanayokumbana nayo ni ya mipaka, kati ya vijiji na vijiji pamoja na ile ya mipaka ya vijiji na hifadhi za Taifa. Hata hivyo, amekiri kuwa changamoto hizo wanazokumbana nazo ndio hasa lengo la kazi hiyo, hivyo kwa kuchukua muda kuitatua ndio mafanikio ya kazi kwani malengo yanatimia.

Wilaya ambazo baadhi ya vijiji vyake vimemaliza kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ni Karatu, Kondoa, Bunda na Simanjiro ambapo jumla za Hatimiliki za Kimila 350 zimeandaliwa na zinatarajia kutolewa kwa wananchi wanaomiliki ardhi kwenye vijiji hivyo. Aidha, kazi hiyo bado inaendelea kwenye Wilaya za Tarime, Simanjiro, Bariadi na Mbulu ikiwa na matarajio ya kufikia vijiji 95 ifikapo Juni 2019.

Kazi hii ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha Hifadhi za Taifa zinaendelea kuwepo kwa ajili ya maendeleo ya nchi pamoja na jamii zinazoishi kuzunguka hifadhi hizo zinanufaika kwa namna moja au nyingine kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ambapo kama ikitekelezwa, kama vile kwa kufanya shughuli ambazo ni rafiki na uhifadhi, zitasaidia kuondoa migogoro ambayo imekuwa ikiibuka mara kwa mara pamoja na kuinua maisha ya jamii hizo.