Habari
Mkurugenzi Mkuu NLUPC atembelea Nanenane, ashiriki kutoa Elimu

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Dkt. Stephen J. Nindi ametembelea na kutoa elimu kwa wananchi na wadau katika maonesho ya 28 ya NaneNane Kanda ya Kati yanayoendelea katika viwanja vya maonesho vilivyopo Nzuguni, jijini Dodoma.
Akiwa katika sehemu ya banda la Tume lililopo kwenye banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ameshiriki kutoa elimu kwa wadau wakiwemo watumishi wa umma kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali juu ya uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
Akielezea juu ya changamoto ya utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, Dkt. Nindi amesema kikwazo kikubwa ni kukosekana kwa uwekezaji mkubwa na ushirikiano baina ya sekta zote zinazohusika na rasilimali ardhi. Aidha, Mamlaka za upangaji kutoipa kipaumbele uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni sababu mojawapo inayofanya kutotekelezeka kwa mipango ya matumizi ya ardhi.
“Sekta ya ardhi inahitaji uwekezaji mkubwa na kwa ushirikiano na sekta nyingine ili tufanikiwe, tuwekeze rasilimali mbalimbali ikiwemo watu, fedha, muda na nyinginezo, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi na Mashirika ya maendeleo, alisema Dkt. Nindi.
Vilevile Mkurugenzi Mkuu aliwakumbusha wataalamu wanaowezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kuegemea zaidi kwenye sayansi ya uandaaji wa mipango kuliko kufaya kazi kwa mazoea ambapo hupelekea kubariki matumizi yaliyopo.
“Ule mpango kazi wa jamii (Community Action Plan) unatakiwa uandaliwe kisayansi, kwani ndio nyezo muhimu katika utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, hivyo wataalamu kule Wilayani, wanatakiwa kulizingatia hili kwani ndio jambo litakalosaidia wakati wa utekelezaji wa mipango ya matumzi ya ardhi,” alieleza Dkt. Nindi.
Katika maonesho hayo yenye kaulimbiu “Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, chagua viongozi bora 2020”, Tume imejikita zaidi katika kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (NLUFP) ambao umebeba programu mbalimbali za utekelezaji wake zikiwemo za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Maonesho hayo yanayohusisha wadau mbalimbali Serikalini na sekta binafsi yaliyoanza tarehe 01/08/2020 yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mh. Suleiman Jafo na yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 10/08/2020.