Habari
Ushirikiano mpya Waibuka kati ya Tume na Chuo Kikuu cha TWENTE katika Sekta ya Ardhi
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imefanya kikao cha ushirikiano kwa njia ya mtandao na Chuo Kikuu cha Twente cha Uholanzi, kupitia Kitivo cha Geo-Information Science and Earth Observation (ITC), kwa lengo la kujadili maeneo ya ushirikiano katika Utafiti, Mafunzo na matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye sekta ya upangaji na usimamizi wa ardhi.
Katika kikao hicho, Chuo Kikuu cha Twente kiliwasilisha maeneo mbalimbali ya utafiti yanayotekelezwa na Kitivo hicho, ikiwemo matumizi ya teknolojia za anga (earth observation), modeli za kidijitali (digital twins), usimamizi wa ardhi kwa njia shirikishi, na matumizi ya teknolojia za GIS na 3D modelling katika kuimarisha upangaji wa ardhi, Mijini na Vijijini. Vilevile, chuo hicho kilieleza uwezo wake katika kutoa mafunzo ya muda mfupi, kozi maalum, na programu za umahiri kwa njia ya ushirikiano.
Aidha, Twente iliainisha uwezo wake mkubwa katika kutengeneza na kutumia zana za kidijitali zinazosaidia maamuzi ya kupanga ardhi, ikiwemo matumizi ya ‘map tables’ na mifumo ya digital planning. Zana hizo zimekuwa zikisaidia kuleta pamoja wadau mbalimbali, kurahisisha maamuzi ya pamoja, na kuongeza ufanisi katika maandalizi ya mipango ya matumizi ya ardhi.
Alkadharika, wataalamu wa chuo hicho walieleza kuhusu uzoefu wa chuo hicho katika kutekeleza miradi ya Kimataifa ya usimamizi wa ardhi, ikiwemo matumizi ya drones, mifumo ya kisasa ya kuhifadhi taarifa, pamoja na programu za kujengea uwezo watumishi wa sekta za umma katika nchi mbalimbali.
Kwa upande wake, Tume ilipongeza hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa kufanya needs assessment na capability assessment ili kubainisha maeneo ya kipaumbele kwa ushirikiano, yakiwemo utafiti wa pamoja, mafunzo ya wataalamu, matumizi ya teknolojia za kisasa katika upangaji wa matumizi ya ardhi, na uanzishaji wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa ardhi.
Tume na Chuo Kikuu cha Twente zimekubaliana kuendelea na hatua zinazofuata kupitia mawasiliano ya kuandaa mpango kazi mahsusi wa kuanza kutekeleza maeneo ya ushirikiano, ikiwemo utafiti, mafunzo, na ubunifu wa mifumo ya kidijitali inayolenga kuimarisha huduma za upangaji na usimamizi wa ardhi nchini.
Katika hatua za mwanzo, pande hizo mbili zinatekeleza utaratibu wa kupanga maeneo yatakayotoa matokeo ya haraka (quick wins), ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa programu za mafunzo ya pamoja, uendelezaji wa zana za kidijitali za kutumia katika uchambuzi wa taarifa za ardhi, pamoja na kufanya tathmini ya mahitaji ya kitaalamu na miundombinu ya kisayansi itakayowezesha ushirikiano kuanza kwa ufanisi.
Hatua hii inalenga kuweka msingi imara wa utekelezaji wa shughuli za muda mrefu katika sekta ya utafiti na upangaji wa ardhi. Pia ilipendekezwa kufanyika kwa ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya pande hizo mbili pamoja na maandalizi ya Hati ya Makubaliano (MoU) itakayoongoza ushirikiano huo.
