Habari
Ngorongoro kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Wilaya
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja na Shirika la FZS imeanza zoezi la uandaaji Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ambao utakuwa dira ya ukuaji wa Halmashauri hiyo.
Kazi hiyo itahusisha kufanya tathmini ya rasilimali ardhi zilizopo kwenye eneo lote la Halmashauri hiyo na kuzipangia namna bora zinavyoweza kutumika kwa manufaa ya mwananchi mmoja mmoja, Wilaya na Taifa kwa ujumla.
Aidha, zoezi hilo limeanza kwa kukutanisha wadau wanaohusika na upangaji, usimamzi na utekelezaji wa matumizi ya ardhi ili kupata maoni ya namna ya kupanga matumizi ya ardhi kutokana na rasilimali zilizopo Wilayani.
Akifungua mkutano wa wadau hao, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mh. Raymond Mangwala, amewataka wadau hao kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na ushauri utakaosaidia kufanikisha zoezi hilo muhimu ndani ya Wilaya.
“Mpango huu utakuwa dira ya ukuaji wa Halmashauri yetu, utatoa mwongozo na majibu ya changamoto mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi, hivyo nawaomba tushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na kushauri”, alisisitiza Mh Mangwala.
Vilevile, Mh. Mangwala ameishukuru Serikali kupitia Tume kwa kuwezesha uandaaji wa mpango utakaosaidia kuondokana na changamoto za matumizi ya ardhi.
“Naishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani hili jambo ni agizo lake kwamba maeneo yote hapa nchini yanapaswa kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi na kumilikishwa, na sisi Ngorongoro tumeanza kunufaika mapema na nia hiyo njema ya Serikali”, alisema Mh. Mangwala.
Awali, akitoa utangulizi wa juu ya dhana ya uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tume, Dkt. Joseph Paul aliyekuwa akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu, alisema kuwa, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni takwa la kisheria. Aidha, kwa mujibu wa sheria, mipango ya matumizi ya ardhi huandaliwa na Mamlaka za upangaji na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Soitsambu Bw. Marko Lorru ameishauri Serikali kuendelea na utaratibu wa upangaji matumizi ya ardhi kwani kwa upande wao imekuwa ni fursa ambayo huko nyuma haikuwepo.
“Tupo hapa kwa ajili ya uandaaji mpango wa matumizi ya ardhi, na mimi naona kama ni fursa na ni hatua nzuri tumefikia kwa kuwa kwa muda mrefu toka uanzishaji wa Wilaya yetu, hatujawahi kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi” alisema Bw. Lorru na kuongeza “Serikali iendelee, kwa kuwa huu ni mwendelezo ambapo hapo awali tulianza na uwekaji wa mipaka ya vijiji pamoja na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na sasa tumeanza mchakato wa uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi wa Halmashauri ya Ngorongoro, hii itatuondoa tulipokuwa pagumu, kwenda pazuri”.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ambaye pia ni Mratibu wa PLUM, Bw. Kelvin Aligawesa ameeleza kuwa zoezi hilo ni muendelezo wa kazi iliyoanza mwezi wa 11. Aidha, Bw. Aligawesa aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa Wilaya hiyo, Mpango huo utaisaidia Wilaya kutumia rasilimali ardhi zilizopo katika mgawanyo sahihi kwa mujibu wa matakwa ya sekta mbalimbali.
“Sasa hivi tupo kwenye zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi wa Halmashauri nzima, ambapo litatuwezesha kujua namna gani rasilimali ardhi zitumike kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu na pamoja na uhifadhi. Kwa sasa tupo katika hatua ya ushirikishwaji wa wadau kwa ajili ya kupokea maoni na ushauri na kisha tutaenda uwandani (field) kuyafanyia kazi hayo maoni na kisha tutakuwa na rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi” alisema Bw. Aligawesa.
Kuwepo kwa mkutano wa wadau wanaohusika na usimamizi na utekelezaji wa matumizi ya ardhi ni hatua mojawapo iliyoainishwa kwenye Mwongozo wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya. Aidha, kwa mujibu wa Mwongozo huo, unazitaka Mamlaka za upangaji kuzingatia ushirikishwaji wa watumiaji ardhi katika eneo husika pamoja na kutambua maslahi yao katika hatua zote za upangaji.
Mkutano huo wa siku moja uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ulihusisha viongozi wa Wilaya, Halmashauri, Kata na Vijiji. Vilevile, wadau wengine walioshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka kwenye Taasisi za Serikali, Mashirika binafsi pamoja na Asasi za Kiraia.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mh. Raymond Mwangwala (aliyesimama) akifungua Mkutano wa Wadau kwa ajili ya Uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Mkurugenzi wa Utafiti kutoka Tume Dkt. Joseph Paul (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi kuhusu dhana ya uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi ya Wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro (mwenye tai) akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Madiwani walioshiriki katika Mkutano wa Wadau kwa ajili ya Kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Sehemu ya Washiriki waliohudhuria Mkutano wa Wadau kwa ajili ya uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi Bw. Dioscory Kanuthi kutoka Tume (aliyesimama) akiwasilisha mada juu ya Dhana ya Uandaaji, Usimamizi na Utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Mh. Mohamed Festo Bayo akitoa nasaha zake wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wadau kwa ajili ya Uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Mh. James Hamza Masedo, Diwani wa Kata ya Sale akichangia mjadala katika Mkutano wa Wadau kwa ajili ya Uandaaji Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Mwakilishi kutoka Taasisi za Dini akichangia mada wakati wa Mkutano wa Wadau
Mwakilishi kutoka Asasi za Kiraia akichangia Mada katika Mkutano wa Wadau
Picha ya pamoja kati ya Mgeni Rasmi Mh. Raymond Mangwala na Wenyeviti wa vijiji waliohudhuria Mkutano wa Wadau kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.