Habari
Bajeti ya Tume Yaongezeka; Kasi ya Upangaji ya Matumizi Ardhi Kunoga
Bajeti ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika upande wa fedha za miradi ya maendeleo, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya upangaji wa matumizi ya ardhi nchini kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi na kuchochea maendeleo endelevu.
Ongezeko hilo limebainika leo Mei 28, 2026, Bungeni Jijini Dodoma wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Fungu Na. 48) pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (Fungu Na. 03) kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, bajeti ya maendeleo ya Tume imeongezeka kutoka shilingi bilioni 4.5 katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi kufikia shilingi bilioni 48 kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Ongezeko hilo linaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya upangaji wa matumizi ya ardhi nchini.
Hadi sasa, jumla ya Vijiji 4,925 kati ya Vijiji 12,333 nchini vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Kati ya hivyo, vijiji 2,750 sawa na asilimia 55.83 vimeandaliwa mipango hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Akwilapo alimpongeza Mhe. Rais kwa kuongeza fedha za upangaji wa matumizi ya ardhi, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha azma ya dhati ya Serikali katika kumaliza migogoro ya ardhi na kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali za ardhi.
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya upangaji wa matumizi ya ardhi katika Vijiji vyote vilivyosalia, pamoja na kuhakikisha mipango hiyo inazingatiwa ipasavyo. Aidha, Kamati ilibainisha changamoto ya ukosefu wa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi.
Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti uliokuwepo hapo awali, ongezeko la migogoro ya ardhi, pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa upangaji wa matumizi ya ardhi.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mh. Timotheo Mnzava, alieleza kuwa suluhisho la kudumu la migogoro ya ardhi ni kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi. Aliongeza kuwa ongezeko la bajeti ya maendeleo hadi shilingi bilioni 48 ni hatua kubwa ikilinganishwa na bajeti ya awali, na litasaidia kuongeza kasi ya upangaji wa Vijiji zaidi ya 1,490 katika mwaka wa fedha ujao.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kukamilisha hatua zote sita za upangaji wa matumizi ya ardhi na kuhakikisha utoaji wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCRO) kwa wananchi ili kuimarisha umiliki salama wa ardhi.
Ongezeko hilo la bajeti linatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya ardhi kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kupunguza migogoro ya ardhi, na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.
