Habari
Mkurugenzi Mkuu Tume akagua Upangaji wa Ardhi Morogoro, Apongeza Maendeleo
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC), Bw. Joseph C. Mafuru, amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kukagua utekelezaji wa zoezi la uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji tisa vinavyowezeshwa na wataalamu wa Tume hiyo.
Katika ziara hiyo, Bw. Mafuru ametembelea vijiji vya Vuleni, Kikundi, Lukonde, Tambuu, Misaga, Mtombozi, Milegwelengwe na Dakawa, ambapo ameshuhudia hatua mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hilo ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi, utengaji wa maeneo kwa matumizi tofauti ya ardhi, pamoja na uandaaji wa ramani zinazoonesha matumizi ya ardhi katika Vijiji husika.
Akizungumza na wananchi na wataalamu katika maeneo hayo, Bw. Mafuru amepongeza juhudi zinazofanywa na wataalamu kutoka Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, akieleza kuridhishwa na kiwango cha uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Amesema uelewa huo ni matokeo ya ushirikishwaji mzuri wa jamii katika mchakato mzima wa upangaji wa matumizi ya ardhi, jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha utekelezaji endelevu wa mipango hiyo na kupunguza migogoro ya ardhi.
Mkurugenzi Mkuu huyo amewahimiza wataalamu kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi, akibainisha kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Tume itakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini kufuatia ongezeko kubwa la bajeti.
Bw. Mafuru amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuongeza bajeti ya Tume kutoka shilingi bilioni 4.5 hadi bilioni 38, hatua ambayo itawezesha kuandaliwa kwa mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji zaidi ya 1,400 kila mwaka.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa bajeti hiyo utaifanya Tume kuwa na uwezo wa kuhakikisha Vijiji vyote vilivyosalia nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitano ijayo.
Ziara hiyo inaendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro hadi kukamilika kwa shughuli za upangaji wa matumizi ya ardhi katika Vijiji husika.
