Habari

Tume yafanya Mazungumzo ya Ushirikiano na Ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Tongji, China

Tume yafanya Mazungumzo ya Ushirikiano na Ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Tongji, China
Nov, 26 2025

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) imekutana na ujumbe kutoka Taasisi ya International Cooperation and Consultancy Center (ICCC) iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Tongji cha China kwa lengo la kujadiliana namna ya kuanzisha na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya Utafiti, Upangaji Matumizi ya Ardhi, matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, ikijumuisha dhana ya kuendeleza Vijiji na miji mahiri (Smart Villages & Smart Cities).

Mkutano huo uliofanyika leo Novemba 26, 2025 katika Ofisi za Tume Jijini Dodoma, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Joseph C. Mafuru ambapo katika yake amesisitiza umuhimu wa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu maeneo ambayo Tume na ICCC zinaweza kushirikiana ili kuboresha mifumo ya upangaji na usimamizi wa ardhi, hususan katika matumizi ya teknolojia bunifu, uimarishaji wa mifumo ya ukusanyaji taarifa (data), na kuboresha huduma za upangaji matumizi ya ardhi katika ngazi za Vijiji, Miji na Taifa.

Aidha, Bw. Mafuru ameeleza kuwa moja ya maeneo muhimu ya ushirikiano ni kuendeleza upangaji wa matumizi ya ardhi unaolenga maendeleo ya Vijiji mahiri, unaotumia TEHAMA, mifumo ya kijiografia (GIS), huduma za kidijitali na ubunifu unaochochea uongezaji tija katika matumizi ya ardhi na rasilimali za Vijijini.

Kwa upande wao, Prof. Rocky Wen Xiaoyi na Prof. Min Tang kutoka ICCC wameelezea utayari wa Taasisi yao kushirikiana na Tume katika maeneo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa, uendelezaji wa ardhi kwa kuzingatia mbinu za kijiografia, na kuimarisha mifumo ya upangaji shirikishi.

Vilevile, wataalamu hao wameeleza kuwa China imepiga hatua kubwa katika kuendeleza Vijiji mahiri kupitia matumizi ya teknolojia, na wako tayari kushirikisha Tume uzoefu huo kwa kutoa mafunzo, kubadilishana utaalamu na kufanya tafiti za pamoja.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zimekubaliana kuwa kuendeleza smart villages ni sehemu muhimu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa ardhi, kukuza kilimo cha kisasa, kuwezesha huduma za kijamii kwa njia ya kidijitali, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya Vijijini. Ushirikiano huu unatarajiwa kuimarisha uwezo wa Tume katika kupanga na kusimamia matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na mustakabali wa Taifa.

Mkutano huo umefanyika ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uwezo wa Tume kuratibu Upangaji, Usimamizi na Utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia, ukuaji wa sekta zinazotumia ardhi na mahitaji ya maendeleo endelevu. Tume na ICCC zimeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha ubunifu na matumizi sahihi ya rasilimali ardhi nchini.