Habari

Tume Kanda ya Ziwa yashiriki Maonesho ya Nanenane

Tume Kanda ya Ziwa yashiriki Maonesho ya Nanenane
Aug, 17 2026

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Kanda ya Ziwa inashiriki katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Jijini Mwanza, kwa lengo la kutoa elimu kwa umma na wadau kuhusu umuhimu wa uandaaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.

Kupitia maonesho hayo, Tume inatoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na matumizi bora na endelevu ya ardhi kupitia utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, hususan katika kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na kukuza kipato.

Aidha, wananchi wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kuepuka na kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa kuzingatia mipaka na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali kupitia mipango ya matumizi ya ardhi.

Alkadhalika, wananchi wanaotembelea kwenye maonesho hayo wanapata elimu kuhusu umuhimu wa Hati za Hakimiliki za Kimila (CCROs) katika kuimarisha usalama wa milki za ardhi.

Wakulima na wafugaji wenye hati hizo wanaweza kuwa na uhakika zaidi wa umiliki wa ardhi zao na kutumia fursa zinazotokana na umiliki rasmi wa ardhi katika kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Maonesho hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa Tume kuwasiliana moja kwa moja na wananchi, kutoa elimu kuhusu masuala ya ardhi na kuhamasisha matumizi bora, salama na endelevu ya ardhi kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.