Habari
Wadau wavutiwa na Maeneo ya Kilimo, Malisho yaliyopendekezwa kwenye Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (NLUFP)
Baadhi ya wadau waliotembelea Banda la Tume katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni Jijini Dodoma, wamevutiwa baada ya kuona ramani ya maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji nchini katika Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (National Land Use Framework Plan), wakieleza kuwa utekelezaji madhubuti wa mpango huo unaweza kuwa miongoni mwa suluhisho la migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Wadau hao wameeleza kuwa mpango huo una umuhimu katika kuweka mwongozo wa matumizi ya ardhi kwa sekta mbalimbali, ikiwemo Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na hivyo kusaidia kuweka uwiano katika matumizi ya ardhi kwa shughuli za uzalishaji.
Kwa upande wa sekta ya Kilimo, mpango huo unaelekeza katika kuimarisha uzalishaji wenye tija kwa kuongeza mapato yatokanayo na kilimo, kupunguza umaskini na kuimarisha uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya.
Aidha, utekelezaji wa programu ya kilimo unalenga kuongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo cha mashamba makubwa na wakulima wadogo, kuboresha mifumo ya utunzaji wa mazao pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazofaa katika uzalishaji.
Kwa upande mwingine, Programu ya Mifugo inalenga kuimarisha sekta hiyo kwa kuongeza tija na kipato cha wafugaji na wakulima, kuboresha uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa ajili ya viwanda vya ndani na biashara ya nje, pamoja na kuinua hali ya maisha ya jamii zinazotegemea shughuli za mifugo.
Aidha, programu hiyo inalenga kuimarisha matumizi ya nishati inayotokana na samadi, hatua inayoweza kuchangia matumizi endelevu ya rasilimali na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazojishughulisha na ufugaji.
Kwa ujumla, wadau wameeleza kuwa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi kwa kuzingatia maeneo yaliyopendekezwa kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji utasaidia kuweka matumizi ya ardhi yaliyo wazi na yanayotekelezeka, kupunguza mwingiliano wa matumizi na migogoro, na kuwezesha sekta za kilimo na mifugo kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
