Habari
Ziara ya Tume yafunua mbinu bora za Upangaji na Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi
Katika muendelezo wa ziara ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) ya kuimarisha ushirikiano na University of Twente kupitia Kitivo cha ITC (Faculty of Geo-Information Science and Earth Observation), ujumbe huo umejionea kwa vitendo namna mipango ya matumizi ya ardhi inavyotekelezwa kwa ufanisi katika maeneo mbalimbali nchini humo.
Miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa ni Mji wa Kampen na eneo la Ijsselmeer, ambapo ujumbe ulipata uzoefu kuhusu mbinu za upangaji wa matumizi ya ardhi katika ngazi ya Halmashauri, hususan katika kukabiliana na hatari za mafuriko zinazotokana na kujaa kwa mito. Mifumo ya upangaji iliyopo imewezesha kuunganisha matumizi ya ardhi na mikakati ya kudhibiti majanga, hivyo kupunguza athari kwa jamii na miundombinu.
Aidha, ujumbe ulifanya ziara katika maeneo ya Vijijini ya Mji wa Overijssel, ambapo ulijionea utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika sekta za kilimo na ufugaji. Katika maeneo hayo, shughuli za uzalishaji zimeunganishwa na matumizi ya nishati mbadala pamoja na maendeleo ya Vijiji, hali inayochochea ukuaji wa uchumi huku ikihifadhi mazingira.
Katika hatua nyingine, ujumbe ulitembelea eneo la Roombeek lililopo mjini Enschede, ambalo ni mfano wa upangaji upya wa makazi baada ya janga la moto. Kupitia mbinu za ushirikishwaji wa jamii (participatory development), eneo hilo limepangwa upya kwa kuzingatia mahitaji ya wakazi, usalama na maendeleo endelevu ya miji.
Kwa ujumla, ziara hiyo imeiwezesha Tume kupata uzoefu wa moja kwa moja kuhusu utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika mazingira tofauti ya Mijini na Vijijini pamoja na mbinu za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na majanga.
Uholanzi imeendelea kuonesha mfano bora wa utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi, hali inayotoa fursa muhimu ya kujifunza kwa Tanzania katika kuimarisha upangaji na usimamizi wa rasilimali ardhi.
Uzoefu huo unatarajiwa kuwa chachu kwa Tanzania kuimarisha upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kuzingatia mbinu shirikishi, matumizi ya teknolojia za kisasa na mifumo jumuishi ya usimamizi wa ardhi.
