Habari

Nsimbo kuwa Kitovu cha Kilimo na Ufugaji kupitia Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya

Nsimbo kuwa Kitovu cha Kilimo na Ufugaji kupitia Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya
Sep, 02 2022

Wadau wanaohusika na upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika Halmashauri ya Nsimbo Mkoani Katavi kwa kauli moja wameazimia kutekeleza Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri hiyo kupitia dhana ya Kilimo na Ufugaji ili kuondoa migogoro ya ardhi, kukuza uchumi wa Halmashauri pamoja na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Azimio hilo limefikiwa na Wadau kwenye Mkutano uliofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Msaginya Mkoani Katavi kwa ajili ya kuwasilisha Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya Nsimbo ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Nsimbo.

Awali, akiwasilisha Rasimu ya Mpango huo uliopendekeza dhana tatu za Kilimo na Mifugo, Uhifadhi wa Hewa Ukaa pamoja na Kilimo Misitu, zilizotokana na rasilimali ardhi zilizopo ndani ya Halmashauri hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi (ADLUM) kutoka Tume Bw. Dioscory Kanuthi ameeleza kuwa mpango huo umeandaliwa ili kuiwezesha Halmashauri ya Nsimbo kukua kiuchumi kwa tumia fursa za rasilimali ardhi walizonazo.

“Baada ya mpango huu kukamilika, wananchi na wadau wengine wote wakisimimiwa na Halmashauri watapaswa kushirikiana kuhakikisha kwamba miradi iliyopendekezwa inatekelezwa katika kipindi chote cha mpango wa matumizi ya ardhi ili kutimiza dhamira ya kuifanya Halmashauri ya Nsimbo ikuwe katika dhana ya kilimo na ufugaji kama ilivyopendekezwa na wananchi” alisema Bw. Kanuthi

Nao baadhi ya washiriki wa Mkutano huo wamempongeza hatua ya uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi na kuahidi kuwa chachu ya uhamasishaji na kusambaza elimu juu ya utekelezaji wa mpango huo kwa wananchi. Aidha, washiriki hao wameeleza kuwa uwepo wa mpango huo utasaidia wananchi kutumia eneo dogo la Halmashauri hiyo kwa mpangilio ili liweze kujitosheleza.

“Kwa niaba ya Madiwani wenzangu, mpango huu tumeupokea vizuri na tutaupeleka kwa wananchi wetu kwenye kata zote 12, sasa wananchi wetu wanaelekea kutumia ardhi yao kwa mpangilio jambo litakalosaidia kupandisha thamani ya ardhi yetu na kutuletea faida kwa wananchi” alieleza Mh. Michael Kasanga, Diwani wa Kata ya Nsimbo.

Mpango huo wa matumizi ya ardhi umeandaliwa katika eneo lote la Halmashauri ya Nsimbo lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 14,623 sawa na Hekta 1,462,300. Aidha, uandaaji wa mpango huo umehusisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka taasisi za Serikali na binafsi, Viongozi katika ngazi za Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa, makundi ya kijamii, wananchi na wadau wengine wanaohusika kwa namna moja ama nyingine na uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka 2007, inazitaka Mamlaka za Upangaji kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kuhakikisha kwamba wadau wote katika eneo la Halmashauri wanahusishwa kwa ukamilifu katika mchakato huo. Aidha, Sheria hiyo inasisitiza kuwasilisha rasimu ya mpango wa matumizi ya ardhi kwenye Mkutano wa Wadau wote katika Wilaya hiyo kwa ajili ya majadiliano na marekebisho.

Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mpanda Bw. Kenneth Simuyemba (Katikati) akifungua Mkutano wa Wadau kwa ajili ya uwasilishaji wa Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Nsimbo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda

Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Nsimbo Bw. Jude Shirima (alieyesimama kulia) akiwasilisha Hali Halisi ya Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri hiyo kwa Wadau wa matumizi ya ardhi wa Halmashauri ya Nsimbo


Sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya Nsimbo

Diwani wa Kata ya Machimboni katika Halmashauri ya Nsimbo, Mhe. Raphael Kalinga akitoa maoni yake juu ya kuboresha Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya NsimboAfisa Mtendaji wa Kijiji cha Muungano katika Halmashauri ya Nsimbo, Gift Kanyoni akiwasilisha maoni ya moja ya kikundi kilichojadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika Mkutano wa WadauMwakilishi kutoka Shirika la Uhifadhi la Frankfurt (Frankfurt Zoological Society – FZS) Bw. Hassan Chikira akichangia mada katika Mkutano wa Wadau

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nsimbo Bw. Mohamed Ramadhani akitoa nasaha zake juu ya utayari wa Halmashauri kutekeleza Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri hiyo pindi utakapokamilika na kuidhinishwa na Mamlaka husika.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sitalike Mhe. Adam Chalamila akifunga Mkutano wa Wadau kujadili Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Halmashauri ya Nsimbo.


Moja ya picha ya pamoja ya Mgeni Rasmi na baadhi ya Wenyeviti wa vijiji vya Halmashauri ya Nsimbo waliohudhuria Mkutano wa Wadau kwa ajili ya kupitia Rasimu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Halmashauri ya Nsimbo