Habari

Nyang'hwale Kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji

Nyang'hwale Kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji
Dec, 31 2024

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale Mkoani Geita imeanza kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 vilivyopo katika Kata za Nyabulanda, Nyang’hwale na Shabaka.

Uandaaji huo wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji utahusisha utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi kama vile Kilimo, Malisho, Makazi, Maeneo ya Huduma za Jamii na maeneo mengineyo kulingana na mahitaji ya wananchi katika Vijiji husika.

Lengo la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi katika Vijiji hivyo ni kuwawezesha wananchi kuepuka muingiliano wa matumizi ya ardhi hali inayopelekea kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara na kudhorotesha shughuli za maendeleo.

Aidha, uandaaji wa mipango hiyo, unatarajiwa kuwawezesha wananchi kutumia ardhi zao kwa tija ili kuongeza uzalishaji katika shughuli zao mbalimbali kutokana na elimu watakayoipata wakati wa zoezi hilo.

Zoezi hilo linafanyika kupitia Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi Nchini (Land Use Planning Project) unaotekelezwa na Tume kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Utekelezaji wa Mradi huo umejikita katika Vijiji vilivyopo kwenye Wilaya zinazopitiwa na Miradi ya Kimkakati, Wilaya zilizopo mipakani na nchi jirani, pamoja na Vijiji vyenye Migogoro ya matumizi ya Ardhi.