Habari
Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Ruvuma yaikaribisha Tume kwa Mikono Miwili

Na Halima Salum, Nyasa, Ruvuma
Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Ruvuma Bw. Shadrack Peter Kansimba amepokea na kuwakaribisha wataalamu wa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) wanaotarajiwa kukita kambi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 14 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.
Akizungumza mbele ya wataalamu hao waliofika Ofisi za Ardhi Mkoani humo kwa ajili ya kutambulisha zoezi la uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi Wilayani Nyasa, Kaimu Kamishna Kansimba ameishukuru Serikali kupitia Tume kwa kuleta zoezi hilo Mkoani Ruvuma ambapo anaamini litatua changamoto za migogoro na kuahidi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo.
“Mkoa wa Ruvuma ni moja ya Mikoa inayokumbana na changamoto nyingi za migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi, hivyo kuja kwa zoezi hili kutasaidia kuondoa migogoro na kuongeza idadi ya Vijiji vitakavyokua vimeandaliwa mpango wa matumizi ya ardhi” alisema Bw. Kansimba
Bw. Kansimba aliendelea kusisitiza kuwa, Ofisi ya Ardhi Mkoa itakuwa tayari kutoa wataalamu pindi watakapohitajika ili kushirikiana na wataalamu kutoka Tume na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa endapo itahitajika kuongeza nguvu itakayopelekea kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa.
Wakati huo huo, timu hiyo ya wataalamu kutoka Tume imewasili Wilayani Nyasa, na kuanza moja kwa moja hatua za awali za uandaaji matumizi ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo Timu Shirikishi ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi ya Wilaya (Participatory Land Use Management Team – PLUM).
Katika awamu ya kwanza Vijiji vitakavyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ni Kwambe, Tumbi, Ng’ombo, Chimate, Ng’indo, Ndonga na Kiagara. Aidha, awamu ya pili itakuwa na vijiji vya Mitomini, Mkalawa, Mipotopoto, Kwangwai, Uhuru, Mkili na Nandonga.
Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji katika Halmashauri hiyo ni utekelezaji wa Mradi wa Upangaji Matumizi ya Ardhi uliojikita kwenye Wilaya na Vijiji vinavyopitiwa na Miradi mikubwa ya Kimkakati, Vijiji vyenye Migogoro ya matumizi ya ardhi pamoja na Vijiji vilivyopo kwenye Wilaya za mipakani.