Habari

Rais ateua Mwenyekiti wa Bodi ya Tume

Rais ateua Mwenyekiti wa Bodi ya Tume
Feb, 11 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Joseph Magufuli amemteua Bw. Fidelis Kashumba Mutakyamilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Makamishna wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kwa awamu ya pili baada ya kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka 2019.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imesema kuwa uteuzi wa Bw. Mutakyamilwa ulianza tarehe 17/01/2019 ambapo atahudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Awali, Bwana Mutakyamilwa aliteuliwa kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume mwaka 2016 ambapo aliongoza Bodi hiyo kwa mafanikio katika kipindi chake cha miaka minne.

Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji Matumizi ya Ardhi ya Mwaka 2007, Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio mwenye Mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wa Bodi ya Tume na wajumbe wake huteuliwa na Mh. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika Bodi hiyo, wanapaswa kuteuliwa wajumbe wasiopungua watano na wasiozidi kumi kutoka miongoni mwa sekta za umma, binafsi na za kijamii zinazohusika na ardhi na maendeleo ya makazi, kilimo na mifugo, mipango ya uchumi na maendeleo, nishati au uchimbaji wa madini, mazingira, fedha pamoja na afya.

Sekta nyingine zinazoweza kutoa wa wajumbe wa bodi ni pamoja na viwanda au biashara, Sheria au utekelezaji wa Sheria, Serikali za Mitaa, Maliasili, Uvuvi au Utalii, Rasilimali za maji pamoja na Asasi zisizo za Serikali na Mashirika ya Kijamii. Aidha, kulingana na wadifa wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume anakuwa mjumbe na Katibu wa Bodi hiyo.

Katika kuzingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na usawa wa kijinsia, Sheria ya Upangaji Mipango ya Matumizi ya Ardhi, imemtaka Mh. Waziri atahakikisha kwamba angalau wajumbe watatu miongoni mwao ni wanawake.