Habari

Rais Magufuli ahimiza upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi

Rais Magufuli ahimiza upangaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi
Sep, 12 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amehimiza upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kama nyenzo muhimu katika kutatua migogoro ya ardhi nchini na kuwapongeza Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa kufanya juhudi za kupanga matumizi ya ardhi katika vijiji vyao.

Akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo, Mhe. Rais amewataka wananchi kufuata Sheria katika kufanya shughuli zao zinazohusiana na ardhi.

“Suala lingine ambalo limezugumzwa hapa (na Mkuu wa Mkoa – Mhe Antony Mtaka) na nimeona siku nyingi mnashiriki katika kutatua migogoro na Hifadhi yetu ya Taifa pamoja na wafugaji na wakulima, mipango yenu mnayoipanga ya mipango ya matumizi bora ya ardhi ni muhimu. Alisema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais amewaasa wafugaji kuanza kufikiria ufugaji wa kisasa kwani idadi ya watu na mifugo inaongezeka lakini ardhi bado inabaki kuwa na ukubwa ule ule. Sambamba na hilo, Mhe. Rais ameongeza kuwa ongezeko la watu limefanya shughuli za kilimo kutanuka hivo mahitaji ya ardhi kuwa makubwa kuliko wakati mwingine wowote. Hivyo ili kuishi kwa amani na kuleta uzalishaji wenye tija kati ya wakulima na wafugaji, hawana budi kushirikiana na mamlaka zilizopo katika kupanga matumizi bora ya ardhi.

“Serikali inapenda wafugaji lakini ni lazima tukubali kuwa ufagaji wa sasa lazima tubadilike, wakati tunapata uhuru tulikuwa na ng’ombe milioni 9, leo zipo milioni 30, watu tulikuwa milioni 10, leo tupo milioni 55, lakini ukubwa ardhi upo vilevile, hii ndio changamoto ambapo Taifa inabidi tuiangalie tunalimaje na tunafugaje” Alisisitiza Mhe. Magufuli.

Kwa mujibu wa Sheria ya Upangaji wa Matumizi ya Ardhi Sura 116, Halmashauri za Wilaya zimepewa mamlaka ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya pamoja na ya vijiji kwa kushirikiana na Halmashauri za Vijiji. Hadi sasa, zaidi ya Halmashauri 100 nchini zimejengewa uwezo na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) namna ya kuandaa, kusimamia na kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi.